Michezo

Okoth kuanza mazoezi leo Alhamisi kwa ajili ya Olimpiki

March 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES ONGADI

NAHODHA wa timu ya taifa ya ndondi Nick ‘Commander’ Okoth, anatarajiwa kuanza mazoezi mepesi katika ukumbi wa St Teresa Nairobi leo Alhamisi.

Okoth aliyefuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki yatakayoandaliwa Tokyo nchini Japan kuanzia Julai 24 hadi Agosti 8, amesema kwamba ataanza mazoezi mepesi kwa nia ya kujiweka sawa kabla ya mashindano haya.

“Safari ya kesho hupangwa leo ndiyo sababu najipanga mapema kwa safari ya Tokyo,” akasema mwamba huyu aliyenyanyua medali ya fedha katika mashindano ya Afrika ya kufuzu yaliyofanyika nchini Senegal majuzi.

Okoth aliyeanza mchezo wa ndondi katika ukumbi wa St Teresa chini ya kocha mkuu wa timu ya taifa Musa Benjamin anasema kwamba madhumuni ya kuanza mazoezi katika ukumbi huo ni kurudisha mkono kwa klabu hiyo yake ya zamani baada ya kupata mafanikio katika mchezo huo.

Okoth anayezichapa katika uzito wa unyoya (feather) pamoja na Christine Ongare katika uzito wa fly ndio pekee waliofuzu miongoni mwa mabondia 13 wa kiume na kike waliopeperusha bendera ya taifa nchini Senegal.

Robert Wangila Napunyi (marehemu) aliweka historia kuwa bondia wa kwanza Afrika kushinda medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki yaliyoandaliwa Seol nchini Korea kusini mwaka wa 1988.

Okoth na Ongare wamewekewa matumaini kibao ya kufuata nyayo za mwamba huyo wa zamani kwa kurudi nyumbani na medali ya dhahabu kutoka nchini Japan.

Kwingineko, matokeo mseto yalisajiliwa katika Ligi ya tawi la Magharibi la Shirikisho la Kandanda nchini (FKF), mwishoni mwa wiki iliyopita.

Rock Saints FC ya mkufunzi Patrick Fundia Ilililima Kabras All Stars FC kwa bao 1-0 katika Shule ya msingi ya Mayonje mjini Malava, katika kaunti ya Kakamega.

Katika uwanja wa Shule ya msingi ya Munganga, Roasterman United FC ilitwanga Munganga FC kwa magoli 2-1.

Sleemaz FC chini ya ukufunzi wa Sylvanus Otema ilisajili sare tasa dhidi ya One Acre Fund (OAF) FC.

Scorpion FC ilizamisha Lugusi Boyz FC kwa mabao 2-0 kwenye Shule ya upili ya Wavulana ya Lugusi mjini Mumias. Mjini Busia, Mayenje FC ilifyeka Mungatsi FC kwa magoli 2-0.

Marenga FC ilikusanya pointi tatu za bwerere baada ya Dragon FC kukosa kufika katika uwanja wa Shule ya msingi ya Nyakwaka kucheza mechi hiyo.

 

Habari za ziada na Titus Maero