• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 2:35 PM
Okumbi kuwaita mabeki sita zaidi kuboresha ulinzi wa kikosi cha Rising Stars kabla ya fainali za Cecafa

Okumbi kuwaita mabeki sita zaidi kuboresha ulinzi wa kikosi cha Rising Stars kabla ya fainali za Cecafa

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa Rising Stars, Stanley Okumbi analenga sasa kuita kambini wanasoka sita zaidi watakaoboresha safu ya nyuma ya kikosi chake kinachojiandaa kwa kampeni zijazo za Baraza la Mashirikisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Chini ya Okumbi, chipukizi hao wasiozidi umri wa miaka 20 waliwapepeta Sudan 2-1 katika mechi ya kupimana nguvu iliyochezewa uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Novemba 5, 2020. Siku mbili kabla ya kutandazwa kwa mechi hiyo, Stars walikuwa wamewanyuka Sudan 3-1 katika mechi nyingine ya kirafiki.

Kwa mara ya pili, vijana wa Okumbi walilazimika kutoka nyuma na kuwapiku Sudan ambao watakutana nao kwenye Kundi C wakati kipenga cha kuashiria mwanzo wa fainali za Cecafa kitakapopulizwa nchini Tanzania mnamo Novemba 22. Fainali hizo zimepangiwa kukamilika rasmi mnamo Disemba 6, 2020.

“Tulianza vibaya mechi zote mbili zilizopita na hali hiyo ilichangiwa na utepetevu wa mabeki. Kikosi kinaridhisha sana ila inatulazimu kuifanyia idara ya nyuma kazi kubwa. Mwanzo wa hatua hiyo ni kuwaita kambini madifenda sita ambao watatupiga jeki kabla ya fainali zijazo za Cecafa,” akasema Okumbi.

Stars walijipata nyuma baada ya dakika tatu pekee za ufunguzi wa kipindi cha kwanza kutokana na bao la Yousif Abdelkarim aliyechuma nafuu kutokana na masihara ya mabeki waliotegemewa na Okumbi. Stars walipoteza nafasi tele ambazo wanasoka Selassie Otieno na Enock Wanyama walipata. Walisawazishiwa mwishowe na Wanyama kabla ya Mathew Mwendwa kuzamisha chombo cha wageni.

Mataifa 10 yamethibitisha kushiriki mechi za Cecafa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17 na 20.

Michuano ya kufuzu kwa fainali za AFCON U-20 zimeratibiwa kusakatwa kati ya Novemba 22 na Disemba 6 nchini Tanzania huku zile za U-17 zikipangiwa kutandazwa kati ya Disemba 13-28 nchini Rwanda.

Rwanda almaarufu Amavubi haijawahi kushiriki fainali za AFCON U-17 na U-20 tangu iwe mwenyeji wa fainali za makala ya 2009 na 2011 mtawalia.

Japo chipukizi wa Amavubi U-20 walibanduliwa mapema kwenye hatua ya makundi mnamo 2011, vijana wao wa U-17 waliduwaza wengi kwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za FIFA zilizoandaliwa nchini Mexico mwaka huo.

Hadi kufikia sasa, Rwanda ndiye mwanachama wa pekee wa Cecafa anayejivunia kuwahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia za FIFA.

Mataifa yatakayoshiriki Cecafa U-20:

Somalia, Burundi, Tanzania, Uganda, Sudan Kusini, Sudan, Eritrea, Djibouti, Ethiopia, Kenya na Tanzania (wenyeji).

Mataifa yatakayoshiriki Cecafa U-17:

Burundi, Tanzania, Uganda, Sudan Kusini, Sudan, Eritrea, Djibouti, Ethiopia, Kenya na Rwanda (wenyeji).

You can share this post!

Katibu katika kikaangio kwa kuwanyima ajira vijana wa Pwani...

Kipa Jordan Pickford aambiwa hapajaharibika neno kambini...