OLIMPIKI: Afisa ajitetea kashfa ya mamilioni
Na RICHARD MUNGUTI
KINARA wa timu ya Kenya iliyoshiriki Olimpiki za Rio 2016, Stephen Soi, Jumanne alikana kuhusika na ubadhirifu wowote wa pesa katika kashfa ya Sh55 milioni iliyokumba michezo hiyo.
Aidha, Soi alikiri kwamba bado hajamrudishia Rais Uhuru Kenyatta bendera ya Kenya ambayo alimkabidhi kuongoza kikosi hicho kilichoshinda medali sita za dhahabu.
“Nchi hii ilinyakua medali nyingi zaidi za dhahabu kuliko Olimpiki zingine tangu 1964,” Soi aliambia mahakama ya kesi za ufisadi.
Alimweleza Hakimu Mkuu Elizabeth Juma kwamba, badala ya kupokewa kwa heshima “alilakiwa katika uwanja wa ndege wa JKIA na maafisa wa polisi kama mhalifu. Hadi wa leo sijarudisha bendera ya Kenya niliyopewa na Rais Kenyatta!”
Soi aliongeza huku akipandwa na hasira kortini: “Sikuhusika kamwe na malipo wala sikuwa ajenti wa kununua tiketi za ndege za mashabiki walioandamana na Team Kenya hadi Rio de Janeiro. Mashtaka dhidi yangu hayana msingi na korti yafaa kuyatupa nje.”
Alisema waliohusika na malipo wakati wa michezo hiyo jijini Rio de Jainero, Brazil, ni wakuu wa Kamati ya Olimpiki (Nock).
Soi aliongeza kuwa kashfa hiyo ikitendeka alikuwa amesafiri hadi jijini Rio na hivyo hakuwa nchini.
“Sikuwa nafanya kazi kwa Wizara ya Michezo wala sikuhusika na masuala ya fedha kwa njia yoyote ile,” akasisitiza.
Kesi hiyo inaendelea kusikizwa.