Michezo

Olimpiki: Krop, Kurgat na Kwemoi wajikatia tiketi kushiriki fainali 5,000m

Na GEOFFREY ANENE August 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKENYA wote watatu Jacob Krop, Edwin Kurgat na Rodgers wamefuzu kushiriki fainali mbio za mita 5,000 kwenye Michezo ya Olimpiki mjini Paris nchini Ufaransa mnamo Jumatano, Agosti 7, 2024.

Narve Gilje Nordas kutoka Norway ameshinda kundi hilo kwa dakika 14:08.16 akifuatiwa na Muethiopia Hagos Gebrhiwet (14:08.16), Mbelgiji John Heymans (14:08.33) nao Krop (14:08.73) na Kurgat (14:08.76) wakafunga mduara wa tano-bora kutoka mchujo wa kwanza.

Kufika kona ya mwisho, vita vya kunyakua tiketi vilikuwa vikihusisha karibu watimkaji 10 na kuwalazimu kufyatuka, huku watatu akiwemo mshindi wa nishani ya fedha kwenye Olimpiki za 2020 Mohamed Ahmed kutoka Canada, wakijipata wamejikwaa na kuanguka.

Rodgers Kwemoi alipata tiketi kwa kumaliza nambari sita katika kundi la pili kwa 13:52.51, nyuma ya Jakob Ingebritsen (13:51.59), Muethiopia Biniam Mehary (13:51.82), Mbelgiji Isaac Kimeli (13.52.18), Mwamerika Grant Fischer (13:52.44) na Mganda Oscar Chelimo (13:52.46), mtawalia.

Fainali itakuwa Jumamosi, Agosti 10 usiku wakati Krop, Kurgat na Kwemoi watakuwa mawindoni kuletea Kenya medali ambayo haikushinda mwaka 2016 na 2021.

Thomas Longosiwa ni Mkenya wa mwisho kupata medali ya 5,000m mwaka 2012 mjini London nchini Uingereza.

Wakenya waliovuna medali katika mbio hizo za kuzunguka uwanja mara 12 na nusu ni John Ngugi (dhahabu mwaka 1988) nao Kipchoge Keino (fedha mwaka 1968), Paul Bitok (fedha mwaka 1992 na 1996) na Eliud Kipchoge (fedha mwaka 2008 na shaba mwaka 2004). Edwin Soi na Thomas Longosiwa waliambulia shaba mwaka 2008 na 2012, mtawalia.