Michezo

Olunga afunga bao licha ya waajiri wake Kashiwa Reysol kulazwa 2-1 na Tosu katika Ligi Kuu ya Japan

September 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI Michael Olunga alifunga bao kwa mara nyingine mnamo Septemba 13, 2020 ila akashindwa kushawishi waajiri wake Kashiwa Reysol kuepuka kichapo cha 2-1 kutoka kwa Sagan Tosu katika kivumbi cha Ligi Kuu ya Japan (J1-League).

Olinga kwa sasa anaongoza jedwali la wafungaji bora wa J1 kwa magoli 16 kutokana na mechi 15. Bao lake dhidi ya Tosu lilipatikana katika dakika ya 24.

Ni goli lililoamsha hasira za Tosu ambao walipachika wavuni mabao mawili ya haraka kupitia kwa Daichi Hayashi na Riki Harakawa katika dakika za 45 na 48 mtawalia.

Ushawishi wa Olunga unazidi kuhisika kambini mwa Reysol tangu aongoze kikosi hicho kupanda ngazi hadi J1 mwishoni mwa msimu uliopita.

Katika mchuano wa mwisho ulioshuhudia Reysol wakiwapiga Gamba Osaka 3-0 ligini, Olunga alipachika wavuni bao la kwanza katika dakika ya pili na kufikisha jumla ya magoli 15 kapuni mwake.

Sogora huyo wa Harambee Stars hakuwa sehemu ya kikosi cha Reysol kilichowapokeza Shimizu S-Pulse kichapo cha 2-1 mnamo Septemba 5.

Olunga alitawazwa mchezaji bora wa J1 katika mwezi wa Agosti baada ya kuongoza waajiri wake kusajili msururu wa matokeo ya kuridhisha yaliyowakweza hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Japan kwa alama 26.

“Huenda huu ni mwanzo wa kuja kwa mataji mengi zaidi. Najitahidi mar azote kuhakikisha kwamba waajiri wangu wanaibuka washindi,” akasema Olunga wakati akipokezwa tuzo ya Meiji Yasuda ya Mchezaji Bora katika Ligi Kuu ya Japan kila mwezi.

Mbali na kufisiwa pakubwa na Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa, mwingine aliyemhongera Olunga kwa mafanikio yake katika J1 ni Seneta wa Siaya, James Orengo ambaye kutumia mtandao wake wa Twitter alisema: “Endelea tu kutia fora. Tunakustahi sana na wewe ni jivunio letu.”

Reysol kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Sanfrecce Hiroshima katika mchuano ujao mnamo Septemba 19.

Katika mwezi wa Agosti, Olunga anayefukuzia taji la mfungaji bora wa J1-League alifungia waajiri wake jumla ya mabao sita kutokana na mechi sita.

Hadi alipojiunga na Kashiwa, Olunga alikuwa amesakatia soka klabu za Thika United, Tusker FC na Gor Mahia katika Ligi Kuu ya humu nchini.

Ushawishi wake ugani ulimfanya kuwa kivutio kambini mwa DjurgardensIF ya Uswidi kabla ya kuyoyomea China kuvalia jezi za Guizhou Zhicheng kisha Girona FC nchini Uhispania.

Alifungua ukurasa wake wa mabao mnamo Agosti kwa kufunga bao dhidi ya Nagoya Grampus na kusaidia Reysol kusajili ushindi wa 1-0. Mnamo Agosti 5, Olunga hakuwa sehemu ya kikosi cha Reysol kilichowapepeta Shonan Bellmare 1-0.

Alirejea kikosini mnamo Agosti nane na akafunga bao katika dakika 62 kwenye sare ya 1-1 iliyosajiliwa na Kashiwa dhidi ya Yokohama F. Marions.

Bao lake la dakika ya 88 dhidi ya Cerezo Osaka mnamo Agosti 15 liliwasaidia Reysol kusajili ushindi wa 3-1 ligini.

Siku nne baadaye, alipachika wavuni bao la kwanza katika dakika ya 76 kwenye ushindi wa 3-2 uliosajiliwa na waajiri wake dhidi ya Vissel Kobe inayotiwa makali na nyota wa zamani wa Barcelona, Andres Iniesta.

Mnamo Agosti 23, Olunga hakuwa sehemu ya kikosi cha Reysol kilichoambulia sare tasa dhidi ya Oita Trinita ligini.

Hata hivyo, alirejea ugani kwa matao ya juu katika mechi iliyofuata na akafungia Reysol mabao mawili katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Kashima Antlers.