Olunga aibuka mchezaji bora wa Agosti katika ligi kuu ya Japan
Na GEOFFREY ANENE
NYOTA Michael Olunga atarejea uwanjani leo akiwa na motisha tele ya kutafuta ufanisi zaidi baada ya kuibuka mchezaji bora wa mwezi wa Agosti wa Ligi Kuu ya Japan.
Mshambuliaji huyo Mkenya anayechezea Kashiwa Reysol, amechana nyavu mara 15 katika mechi 14 amechezeshwa kwenye ligi hiyo ya timu 18 msimu huu. Olunga, 26, alipata tuzo ya Agosti baada ya kufunga mabao sita.
Alishukuru Mungu, wachezaji wenzake, makocha, ligi hiyo na hata marefa kwa mafanikio hayo bila kusahau mashabiki.
“Ni heshima kubwa kuibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora ya mwezi wa Agosti ya Meiji Yasuda Konami 2020. Kwanza, natoa shukrani zangu kwa Mungu kwa neema zake za milele. Pili, wachezaji wenzangu, benchi ya kiufundi, maafisa wengine wasaidizi na mashabiki kwa kunipatia msukumo wa kutafuta ufanisi. Asanteni,” alisema kwenye ukarasa wake wa Facebook.
Olunga anatarajiwa kuanzishwa na kocha Mbrazil Nelsinho wakati Kashiwa itazuru Sagan Tosu leo usiku. Kashiwa, ambayo inashikilia nafasi ya sita kwa alama 26, italenga kumaliza nuksi za kutoshinda nambari 15 Sagan katika mechi nne zilizopita.
Naye kipa Arnold Origi,36, alikuwa michumani timu yake ya HIFK Fotboll ikipepeta wageni wake HJK Helsinki 4-3 kwenye Ligi Kuu ya Finland, Ijumaa.
HIFK haikuwa imepata ushindi dhidi ya HJK katika mechi tisa mfululizo kabla ya kuvuna alama tatu muhimu zilizoindoa kwenye mduara hatari wa kutemwa. Baada ya michuano 13, HIFK ina alama 22. Inashikilia nafasi ya tano.
Nao Clarke Oduor (Barnsley, Uingereza), Johana Omolo (Cercle Brugge, Ubelgiji) na Eric Johana Omondi (Jonkopings Sodra, Uswidi) wanatarajiwa kuchezea timu hizo zao dhidi ya Luton, Anderlecht na Degerfors hapo Jumapili, mtawalia.