Olunga apata mabao mawili Kashiwa ikilima Yokohama
Na GEOFFREY ANENE
MICHAEL Olunga ameimarisha matumaini yake ya kuibuka mfungaji bora kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Japan (J1 League) baada ya kupachika mabao mawili timu yake ya Kashiwa Reysol ikichabanga wenyeji Yokohama FC 3-0 Jumamosi.
Mshambuliaji huyo Mkenya mwenye umri wa miaka 26, sasa ana magoli 19 kutokana na mechi 20 ambazo Reysol imesakata kwenye ligi hiyo ya klabu 18 msimu huu wa 2020.
Aliingia mechi hiyo akiwa amefunga mabao 17, magoli sita mbele wapinzani wake wa karibu Mbrazil Everaldo (Kashima Antlers), Mjapani Yu Kobayashi (Kawasaki Frontale) na Mbrazil Marcos Junior (Yokohama F. Marinos) naye Mjapani Kyogo Furuhashi wa Vissel Kobe alikuwa ametikisa nyavu mara 10.
Katika kampeni yake ya hivi punde, Olunga, ambaye atakosa mechi ya kirafiki ya Kenya dhidi ya Chipolopolo ya Zambia jijini Nairobi hapo Oktoba 13, alifungua ukurasa wa magoli dakika ya tano baada ya kumegewa pasi safi kutoka kwa Mbrazil Cristiano.
Mkenya huyo alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 33 kwa kucheza visivyo kabla ya kuongeza bao la pili dakika ya 76 alipopokea pasi nyingine nzuri kutoka kwa Naoki Kawaguchi ambaye pia alichangia pasi iliyofungwa na Hidekazu Otani dakika ya mwisho mbele ya mashabiki 4, 571 uwanjani Mitsuzawa.
Baada ya kupiga Yokohama FC, Kashiwa sasa imeruka kutoka nafasi ya nane hadi tano kwa alama 33. Kawasaki inaongoza kwa alama 56 baada ya kusakata mechi 21 ikifuatiwa na Cerezo Osaka (42) na FC Tokyo (41) na mabingwa watetezi Yokohama F. Marinos (34) ambao wamecheza mechi 22 kila mmoja.
Olunga atakutana na shujaa wa Uhispania Andreas Iniesta katika mechi ijayo hapoOktoba 10 wakati Kashiwa itaalika Vissel Kobe uwanjani Hitachi Kashiwa.