Michezo

Olunga arejea kwa matao ya juu na kusaidia Kashiwa Reysol kulaza Gamba Osaka 3-0 katika Ligi Kuu ya Japan

September 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI wa Harambee Stars, Michael Olunga alirejea ugani kwa matao ya juu na kufunga bao moja katika ushindi wa 3-0 uliosajiliwa na waajiri wake Kashiwa Reysol dhidi ya Gamba Osaka katika Ligi Kuu ya Japan (J1-League) mnamo Septemba 9, 2020.

Olunga, ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Gor Mahia, alisazwa nje ya kikosi cha Reysol katika mechi mbili za awali dhidi ya Shimizu S-Pulse na Osaka Cerezo.

Alipangwa katika kikosi cha kwanza dhidi ya Osaka na akapachikwa wavuni bao la kwanza baada ya dakika ya pili ya ufunguzi wa kipindi cha kwanza.

Bao hilo lilikuwa la 15 kwa Olunga kufunga katika kipute cha J1-League hadi kufikia sasa msimu huu.

Mabao mengine ya Reysol katika mchuano huo dhidi ya Osaka yalifumwa wavuni kupitia kwa Ataru Esaka katika dakika za 40 na 62 mtawalia.

Ushindi huo ulisaidia Osaka kupaa hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la timu 18 kwenye J1-League. Kikosi hicho kwa sasa kinajivunia alama 26 kutokana na mechi 15 zilizopita. Kwa upande wao, Osaka wanasalia katika nafasi ya nane kwa alama 23 kutokana na maechi 14 zilizopita.

Harambee Stars wanamtazamia Olunga, ambaye pia amewahi kuchezea Thika United, Tusker, Djurgardens IF (Uswidi) na Girona FC (Uhispania), kuongoza kampeni zao za kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Cameroon mnamo 2021.

Olunga atakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na kocha Francis Kimanzi katika mechi za kufuzu kwa fainali hizo dhidi ya Comoros, Togo na Misri baadaye mwaka huu 2020.

Katika mahojiano yake na Taifa Leo hivi majuzi, Nick Mwendwa ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), alisema kwamba Olunga yuko katika fomu ya kuridhisha zaidi ndiposa anaongoza jedwali la wafungaji bora katika soka ya Japan.

Mwendwa alimtaja Olunga kama nguzo na mhimili utakaotegemewa pia na Stars katika mechi mbili za kirafiki ambazo timu ya taifa imepangiwa kushiriki katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kabla ya kuvaana na Comoros.

Resyol wameratibiwa kuvaana na Sagan Tosu katika mchuano wao ujao katika J1-League mnamo Septemba 13, 2020.