Michezo

Olunga: Burundi itatusumbua kuliko Ivory Coast katika kufuzu kwa Kombe la Dunia

June 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CECIL ODONGO

NAHODHA wa timu ya taifa ya soka Harambee Stars, Michael Olunga, amesema itakuwa mtihani mkubwa kukabili Burundi ikilinganishwa na Cote d’ivoire (maarufu Ivory Coast) katika michuano ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 wiki ijayo.

Kenya itachuana na Burundi hapo Juni 7 kabla kuvaana na Ivory Coast Juni 11 katika uwanja wa Mbingu Mutharika jijini Lilongwe, Malawi.

Timu nyingine kwenye kundi hilo ni Gabon, Gambia na Ushelisheli.

Katika mechi mbili zilizochezwa Novemba mwaka uliopita, Kenya ilishindwa 2-1 na Gabon kabla kuibuka na ushindi mnono wa 5-0 dhidi ya Ushelisheli.

Kenya ilihiari kuchezesha mechi hizo mbili ugenini kwa sababu uwanja wa Kasarani ambao unasitiri mashabiki 60,000 unaendelea kufanyiwa ukarabati kwa ajili ya Kombe la Afrika 2027.

Pia uga wa Nyayo wenye uwezo wa kusitiri mashabiki 30,000 unaendelea kukarabatiwa kwa ajili ya CHAN mnamo Septemba mwaka huu.

Kikosi cha wachezaji 25 kinatarajiwa kuondoka nchini kesho jioni hadi Lilongwe, safari ambayo itachukua saa mbili na dakika 18.

Olunga jana alisema kuwa japo mashabiki wanatamani kuwaona wakitandika Ivory Coast, kazi kubwa ni kupata alama zote tatu kila mechi.

“Kundi letu bado lipo wazi na lazima tujitume sana. Kila mtu anazungumzia Cote d’ivoire na kudharau Burundi, ambao wana mtindo wa kucheza kama sisi na ni wapinzani wakali. Lazima tumakinike tupige Burundi ndipo tufikirie ya Cote d’ivoire,” alisema Olunga baada ya mazoezi ya timu hiyo uwanjani Police Sacco mtaani South C, Nairobi, jana.

“Tunaheshimu pia Ivory Coast kama mabingwa wa Afrika ila Burundi pia watakuwa wapinzani hatari. Tusiwapuuze kwani walilaza Gabon,” alieleza straika huyo wa klaby ya Al Duhail nchini Qatar.

Olunga alifunga mabao matano katika mashindano ya mataifa manne yaliyofanyika Malawi mnamo Machi.

Pia alitinga mawili kwenye ushindi wa 5-0 dhidi ya Ushelisheli mnamo Novemba 20.

Mwanadimba huyo ameomba serikali iharakishe ukarabati wa Kasarani na Nyayo ili watumie nyuga hizo katika mechi zijazo za mchujo baada ya Burundi na Ivory Coast.

Kocha Engin Firat katika kikao na wanahabari jana alitangaza kuwa atakosa wachezaji tegemeo Masoud Juma, Joseph Okumu na Erick Marcelo kikosini kwani wote wako nje kutokana na majeraha.