Olunga kucheza dhidi ya Hiroshima
Na GEOFFREY ANENE
NYOTA Michael Olunga anatarajiwa kurejea uwanjani kutafuta bao lake la 17 kwenye Ligi Kuu ya Japan msimu huu wakati Kashiwa Reysol itaalika Hiroshima, Jumamosi.
Mshambuliaji huyo Mkenya alipitisha mabao 15 hapo Septemba 13 Kashiwa ikipoteza 2-1 dhidi ya Sagan Tosu, idadi ambayo washindi wa kiatu cha dhahabu wa msimu uliopita Marcos Junior na Teruhito Nakagawa walifungia Yokohama Marinos ikitwaa taji.
Olunga,26, ambaye alifungia Kashiwa mabao 27 mwaka 2019 ikiingia Ligi Kuu, anaongoza ufungaji wa mabao kwenye ligi hiyo ya klabu 18 baada ya kucheka na nyavu mara 16 katika mechi 15 ameichezea ligini msimu huu.
Yuko mabao sita mbele ya nambari mbili Mbrazil Everaldo (Kashima Antlers) nayo nambari tatu inashikiliwa na Marcos Junior (Yokohama Marinos), Yu Kobayashi (Kawasaki Frontale) na Leonardo (Urawa Red Diamonds) ambao wametikisa nyavu mara tisa kila mmoja.
Dhidi ya nambari 10 Hiroshima, Kashiwa, ambayo iliajiri Olunga mwezi Agosti 2018, itakuwa ikitafuta kulipiza kisasi nyumbani baada ya kulemewa 1-0 Aprili 2018. Itaruka kutoka nafasi ya saba hadi tatu ikibwaga Hiroshima nazo Nagoya Grampus, Kashima na Urawa ziteleze dhidi ya Vissel Kobe, Cerezo Osaka na Kawasaki, mtawalia.