Michezo

Olunga mfungaji bora ligi ya Japan

July 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Michael Olunga wa Harambee Stars aliwafungia waajiri wake Kashiwa Reysol bao jingine katika ushindi mnono wa 4-0 waliousajili dhidi ya Urawa Reds katika Ligi Kuu ya Japan (J1).

Bao hilo lilikuwa la pili mfululizo kwa Olunga kupachika wavuni baada ya kupiga jumla ya mechi tatu bila kufanikiwa kutikisa nyavu za wapinzani katika kipute cha J1 kilichorejelewa mwishoni mwa Juni 2020 baada ya kusitishwa mwezi Machi kutokana na janga la corona.

Ushindi huo uliovunwa na Reysol uwanjani Saitama ulikuwa pia wa pili mfululizo kwa waajiri hao wa Olunga kusajili tangu waipepete Shonan Bellmare 3-2 mnamo Julai 18.

Reysol waliokuwa wageni wa Urawa, walifungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Mbrazil, Richardson Fernandes kabla ya Olunga kufunga la pili. Bao hilo la Olunga katika dakika 51, lilikuwa lake la nne msimu huu na lilitokana na ushirikiano mkubwa kati yake na kiungo Taiyo Koga. Magoli mengine ya Reysol yalitiwa wavuni kupitia kwa Hayato Nakama na Yuta Kamiya.

Kwingineko, Mkenya Clarke Oduor, 21, alitokea benchi katika kipindi cha pili na kufungia Barnsley bao la ushindi katika dakika ya 91 na hivyo kuwachochea waajiri wake kuzamisha chombo cha Brentford 2-1 uwanjani Griffin Park.

Ushindi huo uliwaepushia Barnsley shoka la kuteremshwa ngazi kwenye Ligi ya Daraja la Pili nchini Uingereza (Championship).

Oduor ambaye alizaliwa katika Kaunti ya Siaya, alihamia Uingereza katika umri mdogo kabla ya kusajiliwa na Leeds United waliomtegemea pakubwa katika akademia yao. Ilikuwa hadi mapema 2007 ambapo alitia saini mkataba wa kitaaluma na kikosi hicho ambacho kwa sasa kitashiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu ujao baada ya kutawala soka ya Ligi ya Daraja la Pili (Championship) chini ya kocha Marcelo Bielsa.

Oduor aliingia katika sajili rasmi ya Barnsley almaarufu ‘The Tykes’ mnamo 2019 baada ya kutia saini mkataba wa miaka minne unaotazamiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa 2023. Kuponea kwa Barnsley kulishuhudia klabu za Charlton Athletic, Wigan Athletic na Hull City zikishushwa daraja kwenye Championship hadi Ligi ya Daraja la Tatu kwenye soka ya Uingereza muhula ujao.