• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 3:59 PM
Olunga na Kashiwa Reysol kurejelea mazoezi Novemba 18

Olunga na Kashiwa Reysol kurejelea mazoezi Novemba 18

Na GEOFFREY ANENE

KASHIWA Reysol anayochezea mshambuliaji Michael Olunga itarejea mazoezini Novemba 18 baada ya kukumbwa na visa 15 vya maambukizi ya virusi vya corona.

Ripoti nchini Japan zinasema kuwa Kashiwa itasakata mechi yake ya kwanza mnamo Novemba 21 dhidi ya Sagan Tosu. Ilisimamisha shughuli zake zote Novemba 3 kutokana na visa hivyo vingi vya corona kambini mwake. Mechi dhidi ya Sagan itakuwa nyumbani kwa Kashiwa.

Mnamo Novemba 4, Kashiwa ilitangaza kuwa kikosi chake chote kinaingia karantini katika hoteli moja mjini Chiba kwa siku 10.

Kocha Mbrazil Nelsinho Baptista ni mmoja wa watu 15 kutoka timu ya kwanza ya Kashiwa waliothibitishwa kuwa na ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na virusi hivyo.

“Mazoezi yetu yataanza tena Novemba 18!!!” klabu hiyo ilitangaza Alhamisi kupitia mtandao wake wa Twitter kabla ya kuongeza kuwa Nelsinho huenda pia akarejelea majukumu yake siku hiyo.

Mara ya mwisho Kashiwa ilikuwa uwanjani kabla ya kusitisha shughuli zake ilikuwa Oktoba 31 ilipotoka 0-0 dhidi ya Shimizu S-Pulse ywanjani Hitachi Kashiwa. Olunga aliachwa nje kabisa ya kikosi cha mchuano huo.

Mara ya mwisho Olunga alisakatia Kashiwa ilikuwa Oktoba 28 wakati alimegea Mbrazil Cristiano pasi mbili zilizozalisha magoli katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya FC Tokyo.

Mshambuliaji huyo wa kati anaongoza ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Japan baada ya kuona lango mara 23. Mshindani wake wa karibu ni Mbrazil Everaldo ambaye amefungia Kashima Antlers mabao 14.

Kashiwa inashikilia nafasi ya 10 baada ya kuzoa alama 41 kutokana na michuano 26 kwenye ligi hiyo ya klabu 18. Mechi zake za ligi dhidi ya Vegalta Sendai (Novemba 3) na Oita Trinita (Novemba 14) pamoja na fainali ya Kombe la Levain dhidi ya FC Tokyo (Novemba 7) ziliahirishwa kutokana na visa hivyo vya corona. Levain Cup sasa itaandaliwa Januari 4, 2021.

Olunga yuko nje ya mechi za Kenya za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2021 za Kundi G dhidi ya Komoro mnamo Novemba 11 na Novemba 15.

Kenya ilitoka 1-1 dhidi ya wanavisiwa hao jijini Nairobi mnamo Novemba 11. Vijana wa Jacob ‘Ghost’ Mulee wataelekea Komoro hapo Ijumaa kwa mechi ya marudiano itakayochezwa Novemba 15.

  • Tags

You can share this post!

Mbona mapasta huwabaka waumini?

Washtakiwa kuhadaa watu watawatafutia ajira Kuwait