Michezo

Olympique Lyon ya Ufaransa yaendeleza ubabe dhidi ya Man-City katika kivumbi cha UEFA

August 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MATUMAINI ya taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kusalia nchini Uingereza msimu huu yalizimwa Jumamosi usiku baada ya Olympique Lyon ya Ufaransa kubandua Manchester City waliopigiwa upatu kunyanyua ufalme huo kwa mara ya kwanza katika historia.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walijibwaga ugani kwa minajili ya gozi hilo lililosakatiwa jijini Lisbon, Ureno wakitazamiwa kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakiwadengua miamba wa Uhispania, Real Madrid kwa jumla ya mabao 4-2 kwenye hatua ya 16-bora.

Hata hivyo, Guardiola atasalia kujilaumu kwa kupanga kikosi kilichocheza kwa tahadhari kubwa dhidi ya Lyon ambao hatimaye walizamisha chombo chao kwa kichapo cha 3-1 kwenye robo-fainali hiyo ya mkondo mmoja.

Ni matokeo yaliyoendeleza nuksi ya Man-City kwenye kivumbi hicho na kumwacha Guardiola akiuma meno baada ya kupoteza fursa maridhawa ya kuwaandikia waajiri wake historia katika soka ya bara Ulaya muhula huu.

Tangu awaongoze Barcelona na Bayern kusonga mbele kwenye robo-fainali saba za UEFA, Guardiola ameshuhudia waajiri wake Man-City wakiondolewa kwenye hatua hiyo katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita.

Mwanzoni mwa msimu huu, Guardiola alikiri kwamba atakuwa amefeli pakubwa iwapo atabanduka uwanjani Etihad bila ya kuwaongoza Man-City kutia kapuni taji la UEFA. Mhispania huyo aliyetua uwanjani Etihad mnamo 2016, anajivunia kushindia Man-City mataji sita yakiwemo mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (2017-18 na 2018-19).

Baada ya Liverpool kuwapiga kumbo kwenye EPL msimu huu, Man-City waliokuwa washikilizi wa Kombe la FA walibanduliwa na Arsenal kwenye nusu-fainali ya kipute hicho. Taji la pekee walilolitia kabindoni muhula huu ni la Carabao ambao walilitwaa baada ya kupiga Aston Villa 2-1 mnamo Machi 1, 2020.

Lyon kwa sasa watavaana na Bayern Munich ya Ujerumani kwenye nusu-fainali itakayowakutanisha jijini Lisbon mnamo Jumatano. Kivumbi hicho kitatandazwa siku moja baada ya miamba wengine wa soka ya Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG) kuvaana na RB Leipzig ya Ujerumani kwenye nusu-fainali ya kwanza hapo kesho.

Ni mara ya kwanza tangu 2013 kwa nusu-fainali za UEFA kunogeshwa na vikosi kutoka mataifa mawili pekee; yaani Ufaransa na Ujerumani. Katika msimu wa 2012-13, nusu-fainali za kipute hicho zilishuhudia Bayern wakiwabandua Barcelona huku Borussia Dortmund ya Ujerumani ikiwadengua miamba wengine wa Uhispania, Real Madrid.

Wakicheza dhidi ya Man-City, Lyon waliwekwa kifua mbele na Maxwell Cornet katika dakika ya 24. Ingawa Kevin de Bruyne aliwarejesha Man-City mchezoni kunako dakika ya 69, kikosi cha Guardiola kilionekana kuzidiwa maarifa katika kila idara na utepetevu wa mabeki ukampa fowadi wa zamani wa Cletic, Moussa Dembele fursa ya kufungia Lyon mabao mawili ya haraka mwishoni mwa kipindi cha pili.

Kwa mujibu wa wachanganuzi mbalimbali wa soka, kukung’utwa kwa Man-City kulichangiwa kwa hatua ya Guardiola kuchezesha mabeki watano na kuwaacha nje viungo wabunifu kama vile Bernardo Silva, David Silva, Riyad Mahrez na Phil Foden ambao wangetatiza pakubwa ngome ya Lyon.

Hii si mara ya kwanza kwa Lyon kuonyesha ubabe dhidi ya Man-City.

Msimu wa wa 2018/2019 katika awamu ya makundi wakiwa Kundi F Manchester City ikiwa mwenyeji wa Lyon ilishindwa 1-2 na ilipozuru Ufaransa ikatoka sare ya 2-2. Hii ina maana Lyon ikiwa ugenini ilikuwa na ubora wa mabao.