Ombi la Sonko latupwa
Na RICHARD MUNGUTI
OMBI la Tume ya Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) ipewe muda wa miezi sita kumpa Gavana Mike Sonko ushahidi katika kesi inayomkabili ya Sh357m jana lilikataliwa na mahakama ya kuamua kesi za ulaji mlungula (ACC).
Akitupilia mbali ombi lililowasilishwa na kiongozi wa mashtaka Bw James Kihara ,hakimu mwandamizi Bi Eunice Kagure Nyutu alisema, ni miezi minane tangu Sonko ashtakiwe na hajapewa ushahidi kuandaa ushahidi wake.
Hakimu alielezwa na mawakili Cecil Miller na George Kithi wanaomwakilisha Sonko kwamba walikabidhiwa ushahidi ambao hausomeki na usioeleweka.”
“Tutaandaa ushahidi wa Gavana Sonko aje na ushahidi huu usiosomeka na usioeleweka,” alihoji Bw Miller.
Ombi hilo kwamba nakala za ushahidi hazisomeki na kueleweka liliungwa mkono na mawakili Migos Ogambo, Wachira Kibanya, Jack Migambo, Prof Tom Ojienda na Paula Atikuda.
“Ni ukandamizaji haki za washtakiwa kupewa nakala za ushahidi sisizosomeka. Hakuna kesi inayoweza kuendelea bila ushahidi kukabidhiwa washtakiwa. Lazima DPP na EACC wajue kinachowapasa kufanya,”alisema Bw Ogambo.
Mahakama iliambiwa ni kinyume cha sheria na ikaombwa iamuru DPP na EACC wawakabidhi washtakiwa nakala zinazosomeka.
Bi Nyutu aliamuru DPP na EACC wakabidhi washtakiwa nakala zinazosomeka katika muda wa wiki tatu.
Bi Nyutu alisema lazima, washtakiwa wakabidhiwe ushahidi unaosomeka ndipo wajiandae kujitetea kesi itakapoanza kusikizwa.
Kabla ya kutoa uamuzi DPP na EACC wawakabidhi washtakiwa nakala safi za ushahidi mawakili na viongozi wa mashtaka walikabiliana vikali huku wakilaumiana na kudharauliana.
Cheche za maneno zilirushianwa huku wakati mmoja wakili wa Sonko Bw Kithi akimkabili Bw Kihara ikabidi hakimu aingilie kati na kuwatuliza mawakili wote waliokuwa wamemwinukia kiongozi wa mashtaka.
Na wakati huo huo DPP alitamatisha kesi dhidi ya Dkt Patrick Mwangangi aliyeaga miezi miwili iliyopita.
Dkt Mwangangi alikuwa miongoni mwa washtakiwa 17 walioshtakiwa pamoja na Bw Sonko.
Kiongozi wa mashtaka Bw James Kihara aliikabidhi mahakama cheti cha kifo cha Dkt Mwangangi.
Aliaga miezi miwili iliyopita.
Sonko na washtakiwa wenza wamekanusha kutumia vibaya pesa za umma zaidi ya Sh357milioni katika utoaji wa zabuni za ukusanyaji ushuru na miradi mingineyo.
Walikanusha shtaka waliposhtakiwa Desemba 2019 na wako nje kwa dhamana