Michezo

Onkar Rai abeba ubingwa wa duru ya KCB Meru Rally

November 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

DEREVA Onkar Rai amefuta masaibu ya kukosa kukamilisha duru tatu zilizopita za Mbio za Magari za Kitaifa kwa kubeba ubingwa wa duru ya KCB Meru Rally, Jumamosi.

Onkar, ambaye alipata ajali katika KCB Safari Rally akiendesha gari la Skoda Fabia na kujiuzulu akipeleka Volskwagen Polo GTI R5 kwenye duru ya KCB Kilifi Rally na KCB Nanyuki Rally, ametawazwa mshindi wa KCB Meru Rally baada ya kubadilishana uongozi mara kadha na Baldev Chager na Carl Tundo.

Dereva huyo, ambaye alifungua msimu vyema kwa kunyakua taji la KCB Nakuru Rally mwezi Februari, ameibuka mfalme wa Meru Rally baada ya kukamilisha umbali wa kilomita 155 kwa saa 1:28:40.9.

Tundo, ambaye aliponyoka na taji la Nanyuki Rally pamoja na kukamilisha Nakuru Rally na Safari Rally katika nafasi ya pili na Kajiado Rally katika nafasi ya tatu, ameridhika katika nafasi ya pili katika kaunti ya Meru kwa saa 1:30:31.9.

Bingwa wa Safari Rally na Kajiado, Chager, ambaye alikamilisha Kilifi na Nanyuki katika nafasi ya pili, amefunga mduara wa tatu-bora mjini Meru kwa saa 1:31:07.1. Tundo na Chager waliendesha magari ya aina ya Mitsubishi Evolution 10.

Madereva 19 walishiriki mashindano ya KCB Meru Rally yaliyoanzishwa na Gavana wa Meru, Kiraitu Murungi nje ya benki ya KCB tawi la Nkubu. Kutoka orodha hiyo, madereva 11 ndio wamemaliza mashindano.

Bingwa wa Afrika mwaka 2017, 2018 na 2019 Manvir Baryan, ambaye alitawala KCB Kilifi Rally, ni mmoja wa madereva ambao hawakumaliza duru ya Meru.

Baryan alipata ajali katika gari lake la Skoda Fabia na kujiuzulu.