Michezo

Onyo kali la AK ikichagua Wakenya 444 kupimwa dawa za kusisimua kabla ya Riadha za Dunia 2025

Na GEOFFREY ANENE April 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHIRIKISHO la Riadha nchini Kenya (AK) limechagua wanariadha 444 wanaoweza kuwakilisha taifa kwenye Riadha za Dunia mjini Tokyo, Japan mnamo Septemba 13-21, 2025.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari hapo Jumatano, Aprili 2, 2025, shirikisho hilo lilieleza kwa kina nani ataruhusiwa kupeperusha bendera ya Kenya kwenye mashindano hayo ya haiba.

AK imesema kuwa mamia hao ya wanariadha watapimwa dawa za kusisimua misuli ili kuhakikisha wako sawa kwa mashindano kwa kutimiza masharti.

“Kifungu cha 15.5.1-3 cha sheria za Shirikisho la Riadha Duniani dhidi ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli kinasema wanariadha lazima wapimwe mara tatu nje ya mashindano bila ya kupewa notisi kabla ya Riadha za Dunia. Ili kutimiza haya, ni jukumu la mwanariadha kuhudhuria mafunzo yote yanayoandaliwa na Kitengo cha Maadili cha Kimataifa cha Riadha (AIU), Shirika la Kukabiliana na matumizi ya pufya nchini Kenya (ADAK) ama AK na pia kutoa habari sawa kuhusu wanakopatikana wakati wote,” AK imetangaza.

AK imeongeza kuwa wanariadha wanaweza kupimwa ndani na pia nje ya mashindano wakati wowote.

“Kukosa kupimwa ama kukataa kufuata sheria za asasi za kupima na kukosa kupeana sampuli yako kutaathiri uwezo wako wa kuwakilisha taifa,” AK ikaonya na kuwataka wanariadha kuwajibika kwa chochote kile kitapatikana katika miili yao.

Lazima wachunguze dawa na lishe wanayotumia kabla ya matumizi ili kuepuka kuvunja sheria bila kujua, AK ikasema.

Wanariadha wanaweza kualikwa na maafisa wa AK, AIU ama ADAK kuhudhuria semina na semina za kupitia mitandao na lazima wahakikishe wanahudhuria vipindi vyote wamealikwa.

Uchunguzi wa kwanza wa dawa za kusisimua misuli unahitajika kuwa umekamilishwa kufikia Mei 24, 2025.

Mwanariadha yeyote atakayekuwa hajamaliza uchunguzi huu kufikia tarehe hiyo hataruhusiwa kushiriki mashindano hata akipimwa mara ngapi baada ya Mei 24, 2025.

Siku ya mwisho ya kukamilisha vipimo vya nje ya mashindano ni Agosti 29, 2024 saa moja jioni saa za Afrika Mashariki.

“Matakwa haya ni kando na yanayohitaji mwanariadha kuwa ametimiza muda ama umbali wa kufuzu na pia kushiriki mashindano ya kitaifa ya kuchaguliwa ambayo pia yanatumiwa kuamua kama utawakilisha taifa,” ikasema AK, ikisisitiza kuwa yeyote atakayekosa kutimiza mahitaji hayo hatawakilisha taifa.