Orca Swim Club yatawala mashindano ya kuogelea mbio fupi na relays mjini Kiambu
KLABU ya kuogelea ya Orca iliibuka mshindi wa jumla katika mashindano ya kuogelea ya mbio fupi na ‘relays’ yaliyoandaliwa na Chama cha Kuogelea cha Kaunti ya Kiambu (KCAA) mnamo Mei 24-25 katika shule ya Regis Runda mjini Kiambu.
Mashindano hayo yaliyoshuhudia ushindani mkubwa, yalileta pamoja waogeleaji zaidi ya 400.
Miongoni mwa taasisi zilizoshiriki ni pamoja na Woodcreek School, Porterhouse School, Juja St. Peter’s, Orca, Nawiri Swimming Club, USIU Dolphins, na Chuo Kikuu cha Mount Kenya.
Kati ya waogeleaji waliovutia macho ni Barack Laja mwenye umri wa miaka saba kutoka Orca, ambaye alivunja rekodi ya mbio za mita 25 ‘butterfly’ kwa kumaliza umbali huo kwa sekunde 19 akishinda medali ya dhahabu.
Faith Mugweru, 14, kutoka Crawford International School naye alinyakua dhahabu ya 100m Individual Medley kwa dakika 1:34.93. “Nilijua ushindani ungekuwa mkali, kwa hivyo nilijitahidi sana katika mazoezi. Mashindano haya yamenisaidia kujiandaa kwa mashindano yajayo ya Kenya Aquatics Long Course yatakayofanyika Kasarani Mei 31,” akasema.
Katika kitengo cha waogeleaji wenye umri wa miaka 18 na zaidi, Sean Odera,19, kutoka USIU Dolphins aliibuka mfalme wa 50m ‘butterfly’ kwa sekunde 32.34 na akaeleza matumaini ya kufanya vyema zaidi katika mashindano yajayo.
Zaidi ya ushindani, gala hiyo ilihimiza ukuzaji wa vipaji. Nancy Karanja, mzazi kutoka Goldfish Nanyuki, alitoa wito kwa maeneo mengine nchini, hasa eneo la Mlima Kenya, kuiga mfano huo wa kukuza waogeleaji chipukizi.
Kocha mkuu wa Crawford International School, Omar Omari, alisema mashindano hayo yalikuwa muhimu kwa kutathmini maandalizi ya timu yake kabla ya mashindano ya taifa ya Long Course.
Washindi kitaifa watapata nafasi ya kuiwakilisha Kenya katika mashindano ya dunia ya Long Course, Open Water, na Masters yatakayofanyika Singapore Agosti 2025.
Kiongozi wa Mombasa Aquatics na mjumbe wa bodi ya Kenya Aquatics, Kahindo Mureithi, alisifu waandaaji wa mashindano na kuwataka waogeleaji wote wanaostahiki kushiriki mashindano ya taifa. Alisisitiza haki katika mashindano na uteuzi wa timu ya taifa.
Katika matokeo ya vikundi, Crawford International School iliongoza kwa upande wa wasichana kwa medali 46 (16 dhahabu, 13 fedha, 17 shaba), ikifuatiwa na Woodcreek School (15 dhahabu, 3 fedha, 3 shaba), na Orca (13 dhahabu, 6 fedha, 4 shaba).
Kwa upande wa wavulana, Orca iliongoza kwa medali 39 za dhahabu, 19 fedha na 15 shaba. Crawford ilikamata nafasi ya pili kwa jumla ya medali 40 (14 dhahabu, 10 fedha, 16 shaba) huku USIU Dolphins ikimaliza ya tatu ikiwa na dhahabu nane, fedha nane na shaba moja.
Orca ilitwaa ubingwa wa jumla kwa medali 104 (55 dhahabu, 28 fedha, 21 shaba), ikifuatiwa na Crawford (33 dhahabu, 29 fedha, 36 shaba) na Woodcreek (21 dhahabu, 16 fedha, 12 shaba).
Hatua kubwa ya kiteknolojia ilishuhudiwa baada ya KCAA kupata vifaa vya kisasa kupima muda kutoka Amerika, ambavyo vitaboresha usahihi wa muda ukilinganishwa na mfumo wa awali wa kutumia mikono. Gavana wa KCAA, Gedion Kioko, alisifu hatua hiyo kama maendeleo muhimu kwa mashindano ya kuogelea katika eneo hilo.
Mgeni rasmi alikuwa Sara Mose, ambaye ni muogeleaji wa kimataifa mzawa wa Kenya anayeishi Poland. Sara aliiwakilisha Kenya katika Mashindano ya Dunia na Michezo ya Afrika mwaka wa 2024.
Akiwa ameandamana na mama yake Magdalena, Sara aliwatia moyo waogeleaji wachanga kuwa na nidhamu, kujiamini, na kudumu katika juhudi zao. Magdalena alisimulia safari ya miaka 12 ya kujitolea na kuthibitisha kuwa sasa lengo lao ni kuona Sara akifuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Los Angeles 2028.
Katibu Mkuu wa Kenya Aquatics, Collins Marigiri, aliwashukuru wazazi na wadau wa Kiambu kwa kufanikisha gala hiyo. Pia alipongeza kitengo cha kiufundi la KCAA kwa kulea maafisa wapya wa mashindano, jambo linalodhihirisha kujitolea kwao katika kukuza mchezo wa kuogelea nchini.