Michezo

Orlando Pirates ya Afrika Kusini pazuri zaidi kumng'oa Muguna kutoka Gor Mahia

September 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

ORLANDO Pirates ni miongoni mwa klabu nne za Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL)zinazowania huduma za kiungo matata wa Gor Mahia na timu ya taifa ya Harambee Stars, Kenneth Muguna.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Sun nchini Afrika Kusini, wakala wa Muguna ambaye ana makazi mjini Pretoria, Pirates wako pazuri zaidi kuwapiku AmaZulu, SuperSport na Kaizer Chiefs na kujinasia maarifa ya nahodha huyo wa Gor Mahia.

Likimnukuu ajenti huyo ambaye alitaka jina lake libanwe kwa hofu ya kushambuliwa na mashabiki wa Gor Mahia mitandaoni, gazeti la Daily Sun limesema, “Muguna yuko pua na mdomo kuingia katika sajili rasmi ya Pirates.”

Pirates almaarufu ‘Buccaneers’ wana makao makuu mjini Soweto. Walikamilisha kampeni za PSL katika nafasi ya tatu msimu uliopita na kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League). Walitawazwa mabingwa wa CAF Champions League kwa mara ya mwisho mnamo 1995.

Muguna, ambaye angali na miezi 10 pekee kwenye mkataba wake wa sasa na Gor Mahia, amethibitisha kuwa mteja wa wakala huyo anayehusishwa pia na fowadi maarufu mzawa wa Ghana, Asamoah Gyan.

“Nina kipindi kisichozidi mwaka mmoja katika kandarasi ya sasa na Gor Mahia. Sina hofu yoyote kuhusu kikosi nitakachokiwajibikia msimu ujao. Ajenti wangu anayeishi Afrika Kusini anazungumza na vikosi vinne vya PSL,” akatanguliza.

“Nitakuwa nimefanya maamuzi ya ama kusalia Gor Mahia au kutua kwingineko kufikia mwisho wa muhula huu wa uhamisho wa wachezaji. Hata hivyo, dalili zote zinaashiria kwamba nitahama,” akasema nyota huyo wa zamani wa Western Stima.

Iwapo Muguna atafaulu kutua Afrika Kusini, atakuwa Mkenya wa pili katika PSL baada ya kiungo mkabaji wa Harambee Stars, Anthony ‘Teddy’ Akumu aliyesajiliwa na Kaizer Chiefs muhula huu baada ya kuagana na Zesco United ya Ligi Kuu ya Zambia.

Kwa mujibu wa wakala wa Muguna, klabu za DC Motema Pembe (DR Congo), Petro Atletico (Angola) na Azam FC (Tanzania) tayari zimejiondoa kwenye vita vya kumsajili mteja wake.

“Motema Pembe, Atletico na Azam wamethibitisha kukata tamaa katika juhudi za kumsajili Muguna ambaye ataachiliwa tu na Gor Mahia kwa kima cha Sh6 milioni,” akasema.

“Natathmini kwa kina ofa zote za hadi kufikia sasa. Nisingependa kurudia makosa ya mwaka wa 2018 yaliyomshuhudia Muguna akiagana na kikosi cha FK Tirana ya Albania kabla ya mkataba wake kukamilika,” akasema wakala huyo aliyenukuliwa pia na mtandao wa soccernet nchini Ghana.

Muguna aliwahi kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mnamo 2017 akivalia jezi za Stima. Ni ufanisi huo uliomfanya kuwaniwa na Gor Mahia mwanzoni mwa msimu wa 2018.

Katika mahojiano yake ya awali na Taifa Leo, Muguna alikiri kwamba asingechelewa kuikumbatia fursa ya kuingia katika sajili ya kikosi kingine iwapo ofa nzuri ya kuridhisha ingetokea.

“Ningependa kukabiliana na changamoto mpya. Siwezi kutabiri ya kesho kwa sababu ningali na mkataba na Gor Mahia. Kwa sasa ni suala la kusubiri kwa sababu vikosi vitatu vya haiba kubwa kutoka nje ya Kenya vimefichua maazimio ya kunisajili. Hakuna mchezaji asiyevutiwa na ofa nono kwa sababu malipo mazuri ni kiini cha hamasa ya kila sogora,” akaongeza Muguna.