Michezo

Oserian Ladies watiwa adabu tena na Zetech Sparks

September 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Oserian Ladies kwa mara ya pili mfululizo iliangukia pua ilipochomwa magoli 3-1 na Zetech Sparks (Soccer Sisters) kwenye mechi ya kipute cha Soka ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL) iliyochezewa uwanja wa Ruiru Stadium, mjini Ruiru.

Nayo Spedag FC ilinasa ufanisi wa mabao 2-1 dhidi ya Kisumu All Starlets na kulipiza kisasi baada ya kudhalilishwa kwa magoli 9-0 kwenye mechi za mkumbo wa kwanza.

Zetech Sparts ya kocha, Bernard Kitolo ilitwaa pointi tatu muhimu licha ya kulazimishwa kutoka nguvu sawa magoli 2-2 na Mathare United Women (MUW FC) wiki iliyopita.

Nayo Oserian Ladies ilikubali kipigo hicho wiki moja baada ya kutandikwa magoli 7-3 na Kisumu Allstarlets uwanjani Moi Stadium, mjini Kisumu.

Wachezaji wa Trans Nzoia Falcons wanaoshiriki kampeni za Soka la Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL). Picha/ John Kimwere

Vigoli wa Zetech Sparks chini ya nahodha, Puren Anyetu walionyesha mechi safi na kufanikiwa kuandikisha ufanisi huo kupitia juhudi za Yvonne Khavere, Elizabeth Wanyonyi na Puren Anyetu walitikisa wavu kila mmoja mara moja.

Akiongea na Taifa Leo Dijitali, kocha wa Zetech Sparks, Bernard Kitolo alisema ”Baadhi ya wachezaji wangu wamekuwa wakiteswa na majeraha lakini wamepata nafuu ambapo wameanza kufanya kweli pia tunatarajia kuimarisha matokeo yetu kwenye mechi zilizosalia.”

Bao la Spedag FC lilifungwa na Mary Akello huku Merceline Wayodi akisawazishia Kisumu All Starlets kabla ya kujifunga na kuwapa wapinzani wao bao la bwerere lililowasaidia kuzoa alama zote tatu.

Matokeo hayo yalifanya Zetech Sparks kuongezea pointi tatu muhimu na kusalia katika nafasi ya nane kwa alama 32, nane mbele ya Wadadia LG baada ya kucheza mechi 25 na 22 mtawalia. Nayo Kisumu Allstars kwa alama 43 bado inafunga tano bora kwenye jedwali.