• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Palace wazamisha chombo cha Man-United ugani Old Trafford

Palace wazamisha chombo cha Man-United ugani Old Trafford

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United walianza vibaya kampeni ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Crystal Palace uwanjani Old Trafford mnamo Septemba 19, 2020.

Palace walifungua ukurasa wa mabao kunako dakika ya saba kupitia kwa Andros Townsend kabla ya Wilfried Zaha kufunga mengine mawili kunako dakika ya 74 na 85 mtawalia.

Man-United walifutiwa machozi na sajili mpya Donny van de Beek katika dakika ya 80. Bao la Townsend lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Jeffrey Schlupp.

Goli la pili la Palace lilitokana na penalti iliyochangiwa na tukio la beki Victor Lindelof kuunawa mpira wakati akimkabili fowadi Jordan Ayew. Penalti hiyo iliyopanguliwa na kipa wa Man-United kwa mara ya kwanza, ilipigwa upya na Zaha baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba kipa David de Gea alikuwa ametoka kwenye mstari wake wakati ikichanjwa na Ayew.

Ushindi wa Palace ulikuwa mnono zaidi kwa kikosi hicho cha kocha Roy Hodgson kuwahi kujivunia ugani Old Trafford. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Palace kuwabwaga Man-United katika uwanja wao wa nyumbani kwa misimu miwili mfululizo.

Ufanisi huo pia uliendeleza rekodi nzuri ya Palace ambao kwa sasa hawajashindwa katika mchuano wowote ugenini kati ya mitano iliyopita dhidi ya vikosi viwili vya jiji la Manchester.

Vijana wa kocha Ole Gunnar Solskjaer walisuasua pakubwa katika mchuano huo huku baadhi ya wachezaji akiwemo Paul Pogba aliyeondolewa katika kipindi cha pili, wakizembea sana. Nafasi ya Pogba ilitwaliwa na Van de Beek aliyesajiliwa kutoka Ajax ya Uholanzi.

Mchuano huo ulihudhuriwa pia na kocha wa zamani wa Man-United, Sir Alex Ferguson, 78.

Licha ya kuchezea ugenini, Palace walionekana kuwazidi wenyeji wao maarifa katika takriban kila idara huku kwa nyakati fulani, Harry Maguire na Lindelof wakishindwa kuhimili presha kutoka kwa Zaha na Townsend.

Zaha ndiye mchezaji wa mwisho kusajiliwa na Ferguson wakati akiwa mkufunzi wa Man-United mnamo 2013. Hata hivyo, nyota ya mwanasoka huyo raia wa Ivory Coast haikung’aa na akarejea Palace alikotokea mnamo 2015.

Palace kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Everton ugani Selhurst Park katika mchuano wao ujao ligini.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya watakiwa kutoa maoni kuhusu “formula”...

Nketiah ainusuru Arsenal kutoka kwa nyundo la West Ham