• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
Pamzo kuendelea kuwa kocha wa Gor Mahia katika mechi za CAF Champions League

Pamzo kuendelea kuwa kocha wa Gor Mahia katika mechi za CAF Champions League

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Sammy ‘Pamzo’ Omollo ataendelea kusimamia mechi za kimataifa za Gor Mahia na ndiye atakayeongoza kampeni za miamba hao wa soka ya humu nchini dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria katika mechi ijayo ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) mnamo Disemba 23.

Gor Mahia ambao ni mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya wanatarajiwa kuondoka humu nchini mnamo Disemba 19 kuelekea jijii Algiers, Algeria watakakosafiri kwa treni kutoka Tunis, Tunisia baada ya kutokea Cairo, Misri kwa ndege. Mchuano wa marudiano kati ya vikosi hivyo viwili utaandaliwa jijini Nairobi mnamo Januari 5, 2021.

Pamzo ambaye pia amewahi kunoa Tusker, alisimamia mechi za mikondo miwili ya CAF iliyoshuhudia Gor Mahia wakibandua APR ya Rwanda kwenye raundi ya kwanza ya mchujo kwa jumla ya mabao 4-3.

Gor Mahia walipepetwa 2-1 na APR jijini Kigali, Rwanda mnamo Novemba 28 kabla ya kusajili ushindi wa 3-1 katika marudiano yaliyofanyika uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Disemba 5.

Kuteuliwa kwa Pamzo kudhibiti mikoba ya Gor Mahia kwenye CAF kulichochewa na kupigwa marufuku kwa Roberto Oliveira Gonclaves wa Brazil ambaye kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), hakuwa amefuzu kusimamia mechi za kimataifa za CAF.

Oliveira, 60, ameagana tayari na Gor Mahia ambao pia ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya.

Kocha Patrick Odhiambo aliyekuwa msaidizi wa Oliveira, amekuwa akisimamia mazoezi na maandalizi ya Gor Mahia uwanjani Camp Toyoyo, Nairobi. Iwapo Gor Mahia wataangusha Belouizdad na kufuzu kwa hatua ya makundi ya CAF msimu huu, basi watatia mfukoni kima cha Sh58 milioni.

You can share this post!

Beki wa zamani wa Man-United apokezwa mikoba ya ukocha...

Liverpool wadhalilisha Palace kwa kichapo cha 7-0 ligini