Michezo

PANDA CUP: Korea Kusini wakanyaga kombe na 'kulikojolea' baada ya kushinda wenyeji Uchina

May 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA na GEOFFREY ANENE

HEBU fikiria Gor Mahia kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka ya Kenya na katika sherehe zake, kukanyaga kombe na kujifanya kulikojolea.

Hivyo ndivyo Korea Kusini ilifanya ilipochapa wenyeji Uchina 3-0 katika fainali ya soka ya Panda Cup mnamo Mei 29, 2019.

Kwa kawaida washindi hunyanyua kombe wakitwaa ubingwa, hukimbilia nalo uwanjani, hupiga picha nalo hata kulitumia kuteremsha bia jinsi Chelsea walivyofanya baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Uropa.

Hata hivyo, kuna njia ya aibu na ilio na uwezo wa kuhatarisha ushiriki wako katika mashindano mengine jinsi Korea Kusini ilifahamu baada ya mchezaji wake mmoja kukanyaga kombe la Panda Cup ikisherehekea kuibuka mabingwa.

Korea Kusini ilichabanga wenyeji Uchina 3-0 katika fainali Mei 29. Ilikuwa imepiga Thailand 2-1 katika mechi ya ufunguzi Mei 25 na kulemea New Zealand 4-0 Mei 27 katika soka hiyo ya mataifa manne.

Baada ya kushinda taji mjini Chengdu, mabingwa Korea Kusini, ambao walikuwa wamealikwa kushiriki, sasa wamelazimika kuomba msamaha. Hii ni baada ya wachezaji wake kupigwa picha wakisherehekea, huku mmoja wao akikanyaga kombe hilo kwa mguu wake wa kulia.

Uchina imekasirishwa na kisa hiki kisicho cha heshima.

Picha hiyo imesababisha vyombo vya habari nchini Uchina na mitandao ya kijamii kulalamika sana, huku kamati andalizi ya mashindano hayo ikitaja kisa hicho cha Wakorea kuwa “matusi ya hali ya juu.”

Ni hatari kubwa

Shirikisho la Soka la Chengdu lilieleza Korea Kusini iombe msamaha, huku likidokeza kwamba Korea Kusini haitaalikwa tena katika mashindano hayo.

Ripoti zinasema kwamba Wakorea pia walinaswa katika picha moja wakionekana wakijifana kukojolea kombe hilo.

Visa hivi vimefanya Shirikisho la Soka nchini Uchina (CFA) limewasilisha malalamiko kwa Shirikisho la Soka barani Asia kulalamikia kisa cha mchezaji huyo kukanyaga kombe katika makala hayo ya sita.