Partey aeleza sababu zake za kujiunga na Arsenal
Na MASHIRIKA
SAJILI mpya wa Arsenal, Thomas Partey, 27, amesema kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake ni kusaidia Arsenal kurejea “wanakostahili kuwa” na kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Kiungo huyo raia wa Ghana alijiunga na Arsenal mnamo Oktoba 5, 2020 baada ya kushawishiwa kubanduka kambini mwa Atletico Madrid ya Uhispania kwa kima cha Sh6.3 bilioni.
Arsenal wametawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mara 13, wakitwaa ufalme wa taji hilo mara ya mwisho mnamo 2003-04.
“Kila mchezaji anataka kuongoza kikosi chake kutwaa ubingwa na kunyakua makombe yote mengine msimu huu. Hayo ndiyo malengo yangu pia,” akatanguliza Partey.
“Ni kibarua kizito ila tunajitahidi kuhakikisha kwamba tunatimiza maazimio hayo. Tuko tayari kuhimili ushindani,” akasema.
“Hilo ndilo lengo kuu la kikosi na langu pia. Lazima tujitahidi kurejesha Arsenal inakostahili kuwa,” akaongeza.
Tangu watawazwe mabingwa wa EPL, Arsenal wameshinda ufalme wa Kombe la FA mara tano ikiwemo msimu uliopita wa 2019-20 ambapo walipepeta Chelsea 2-1 ugani Wembley mnamo Agosti 2020.
Hata hivyo, waliambulia nafasi ya nane kwenye msimamo wa jedwali la EPL na hawajawahi kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) tangu 2016-17.
“Ni changamoto kubwa ambayo natamani sana kukabiliana nayo, na niko tayari kujitolea kwa udi na uvumba,” akasema Partey aliyeongoza Atletico kutwaa ubingwa wa Europa League na Uefa Super Cup msimu uliopita baada ya kusakata fainali ya UEFA mnamo 2016 dhidi ya Real Madrid.
“Kocha Mikel Arteta na mkurugenzi wa kiufundi Edu wamenifafanulia malengo ya Arsenal pamoja na mipango yao katika kufanikisha maazimio hayo ambayo nimefurahishwa nayo sana,” akaeleza Partey.
Arsenal wameshinda mechi tatu kati ya tano zilizopita za EPL msimu huu wa 2020-21. Kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano jedwalini kwa alama tisa sawa na mabingwa wa 2015-16, Leicester City.
Partey aliwajibishwa na Arsenal kwa mara ya kwanza mnamo Oktoba 17, 2020 dhidi ya Manchester City uwanjani Etihad. Alitegemewa ugani kwa dakika tisa za mwisho katika mechi hiyo iliyoshuhudia Man-City ya kocha Pep Guardiola wakisajili ushindi wa 1-0.