Michezo

PATASHIKA: Desert Foxes na Teranga Lions kukwaana kwenye fainali Afcon

July 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

CAIRO, Misri

MASHABIKI wa Senegal na Algeria walilipuka kwa shangwe baada ya timu hizi kutinga fainali ya Kombe la Afrika (AFCON), Jumapili usiku ambapo sasa zinatarajiwa kucheza Ijumaa.

Teranga Lions ilishinda Carthage Eagles ya Tunisia kupitia bao la kujifunga kutoka kwa beki Dylan Bronn dakika ya 100 uwanjani 30 June nayo Desert Foxes ya Algeria pia ikanufaika na bao la kujifunga kutoka kwa beki William Troost-Ekong katika ushindi wake wa 2-1 dhidi ya Super Eagles ya Nigeria katika uwanja wa kimataifa wa Cairo.

Nyota wa Manchester City, Riyad Mahrez alifungia Algeria bao la ushindi sekunde chache kabla ya kipenga cha mwisho kulia. Nigeria ilikuwa imesawazisha 1-1 kupitia kwa penalti safi kutoka kwa Odion Ighalo.

Baada ya Senegal kujikatia tiketi ya kushiriki fainali ya pili katika historia yake tangu mwaka 2002 ilipopigwa na Cameroon kwa njia ya penalti, mashabiki walifurika jijini Dakar kusherehekea kwa nyimbo na densi.

Sherehe za mabingwa wa mwaka 1990 Algeria zilishuhudiwa katika miji ya Cairo (Misri), Algiers (Algeria), Marseille, Lyon na Paris (Ufaransa) na hata, jijini London nchini Uingereza.

Hata hivyo, mashabiki wa Algeria walikosa ustaarabu. Walisherehekea kupita kiasi.

Polisi nchini Ufaransa walikuwa na kibarua kigumu kudhibiti mashabiki walioamua njia ya pekee kusherehekea ni kuzua fujo.

Ripoti zilisema Jumatatu kuwa zaidi ya mashabiki 280 wa Algeria walikamatwa na polisi waliokuwa wakijaribu kutuliza hali. Polisi walilazimika pia kutumia vitoa machozi kuwatawanya.

Mashabiki walipanda kwenye milingoti ya mabango ya matangazo wakipeperusha bendera ya Algeria, kuimba na kucheza densi na kuwasha fataki.

Mashabiki wengine walianza kurushia polisi chupa na mawe.

Wengine walizuia magari barabarani na kurushia polisi fataki pamoja na kuchoma mapipa ya takataka.

Walitupa pia mabomu ya kutoa moshi. Ripoti kutoka jijini London zilisema kuwa mashabiki wa Algeria waliharibu gari moja la polisi. Pia, waliwasha fataki na kufunga barabara ya Blackstock jijini London.

Inasemekana kuwa usalama uliimarishwa nchini Ufaransa kabla ya nusu-fainali baada ya visa vya makabiliano na uporaji kushuhudiwa Algeria iliposhinda Ivory Coast kwa njia ya penalti 4-3 katika robo-fainali.

Kifo kiliripotiwa nchini Ufaransa baada ya Algeria kuchapa Ivory Coast wakati shabiki wa Algeria alikanyaga mama mmoja gari mbele ya watoto wake.

Katika fainali, Senegal ya kocha Aliou Cisse itatafuta kuwa mshindi wa 15 tofauti wa Afrika.

Kabla ya mwaka 2002, nafasi nzuri ambayo Senegal ilikuwa imemaliza katika AFCON ni nambari nne mwaka 1965 na 1990.

Pia, ilikamilisha katika nafasi ya nne mwaka 2006. Algeria ilimaliza ndani ya mduara wa nne-bora mara sita ikiwemo kuzoa taji mwaka 1990 ilipopiga Senegal 2-1 katika nusu-fainali kabla ya kulemea Nigeria 1-0 katika fainali.