Michezo

PATRICIA KHABUKWI: Refa wa kike mmakinifu mwenye hadhi ya kimataifa

October 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PATRICK KILAVUKA

AKIWA katika Kidato cha Tatu, mwamuzi Patricia Khabukwi alikuwa amelivalia njuga suala urefa na kuchezesha michuano ya vipute mtaani. 

Amejitahidi ukucha kwa jino hadi sasa ni refa wa hadhi ambaye anafanya maaumzi ya kabumbu kama mpuliza kipenga wa kati au muinuaji kibendera katika michuano ya ligi.

Khabukwi alipata fursa ya kuwa mwamuzi baada ya kupata mafunzo maalumu ya urefa kupitia mpango wa mafunzo wa marefa ambao uliandaliwa  na UNICEF.

“Tulipata ya mafunzo ya wiki moja na nikafuzu,” asema refa huyu ambaye alianza urefa kama bado wa mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Kangemi japo masomo ya msingi aliyapata shule za msingi za Kangemi na Kabete Vetlab alikohitimia.

Kipute chake cha kwanza kuchezesha kilikuwa kile kilifadhiliwa na aliyekuwa mgombea wa eneobunge la Westlands Kamlesh Pattini mwaka wa 2007.

Wakati huo alikuwa pia anaichezea timu ya akina dada ya WYSA United chini ya kocha Turncliff Asibela na shule ya sekondari alikosomea kama beki wa kulia au mbeki mkabaji.

Kiu ya kuendeleza taaluma hii kilimpelekea kupandishwa ngazi na kutoa huduma za kuchezesha mpira michuano ya Ligi ya Shirikisho la Kandanda Kenya KFF mwaka 2008 kaunti ndogo ya Westlands.

Mwaka uliofuata nyota yake ilingara zaidi na kuvukishwa daraja hadi kiwango cha kuchezesha Daraja ya Kwanza hadi mwaka 2014.

Anakumbuka kuwa mwamuzi katika mechi za timu kama Sofapaka, Ushuru, Mathare Youth, Bidco miongoni mwa zingine akiwa refa wa kati au mnyanyua kibendera.

Mwaka wa 2015 hakuchezesha gemu yeyote kwa sababu ya shughuli za kifamilia.

Mwaka 2016 alirudia kazi na kuanza kusimamia mechi za ligi ya Shirikisho la Soka Kenya FKF na kutoa huduma zake kwa weledi kama refa wa kati  au muinuaji kibendera.

Kutokana na desturi yake kumakinika sana akiwa uwanjani na kutazama hulka ya wachezaji ugani kutuliza mechi, anasema amepata uungwaji mkono wa mashabiki na wachezaji.

“Ukitaka kusimamia vyema mechi, lazima uwe mwaangalifu tangu mwanzo wa mchuano hadi mwisho. Kama presha imeingia wakati wa mchuano, yakupasa kuituliza kwa kujidhibiti kihamasa ili ufanya maamuzi yafaao.

Isitoshe, ukitoa kadi kila upande unafaa kuridhika kuepusha uchefuchefu wa wachezaji na mashabiki ambao hughadhabika na kuzua taharuki iwapo kadi imepeanwa visivyo,” alieleza mpuliza firimbi huyu.

Kando na kuwa kumpuliza kipenga katika ligi zilizotajwa, yeye huwa katika jopo la kuteua marefa wa kuchezesha misakato ya mchezo ya kandanda shule za upili, kaunti ndogo ya Westlands na kuchezesha michuano ya Kanda ya Nairobi. Fauka ya hayo, yeye ni mwakilishi wa wanawake katika Shirikisho la Soka Tawi la Nairobi Magharibi.

Refa ambaye angependa kumuiga ni  refa wa FIFA Maryanne ambaye huchezesha mechi za Ligi ya Primia.

Anasema baada ya kuwa na uzoefu katika tasnia hii, analenga kuwa msimamizi wa michuano au kuwa refa wa kimataifa.