PATRICK OTIENDE: Straika wa Kangemi anayepania kufikia weledi wa Aubameyang
Na PATRICK KILAVUKA
KUWA na imani na kujiamini kwamba kutumia kipawa cha miguu yake kinaweza kumfikisha katika upeo wa kisoka, kulikuwa kurunzi ya kummulikia njia ya safari yake katika kabumbu.
Sasa yeye ni moto wa kuotewa mbali akicheza kama straika. Ameshiriki ligi kadhaa na kuvumisha kipaji cha kandanda tangu atie guu lake katika fani hii akiwa na miaka kumi na minne shule ya msingi.
Amesukuma kimiani magoli sufufu katika ulingo wa kandanda katika ligi ya FKF, NWRL.
Mwanasoka Patrick Otiende, 24, anapokuwa ugani akitambariza boli na kuachilia mashuti kali, mashabiki hukaa mkao wa kutizama jinsi anavyotesa makipa kwani, anasema nia ya kucheza kama mshambulizi ni kuipa timu yake ushindi na kushirikiana na wachezaji wengine kuimarisha kikosi cha kutandaza boli tamanifu.
Hali hii huvutia mashabiki kushabikia timu ya Red Carpet kipindi chote cha mchezo kwani, hazubaa kuwapa makipa dozi ya makombora mazito yanayowahangisha langoni.
“Mimi huamini kwamba heri kipa auteme au niutumbukize mpira kimiani kwani mshambulizi huaminiwa kwa zana zake dhidi ya wapinzani na kutwaa ushindi,” asema Otiende ambaye alianza kusakata boli akiwa Shule ya Msingi ya Nangili kaunti ndogo ya Likuyani kabla kuendeleza ubabe wake Shule ya Upili ya Kongoni na hatimaye, kuamua kukuza kipawa chake kwa kujiunga na timu ya Carpet baada ya kocha wa timu hii Meshack Onchonga kutembelea eneo hilo la magharibi wakati wa michezo ya Shule za Upili na kugundua utajiri na uwezo wa talanta yake kisha kumsihi agurie Nairobi ili, apanue hema lake la soka na kujijenga kupitia kuchezea timu za hadhi jijini.
Kocha huyo anasema mwaka wa 2007, alitalii kutambua vifaa ambavyo vingejenga msingi wa timu ya Carpet na jicho lake pevu halikukosea pale ambapo lilimuona Otiende na tangu ajiunge na timu, amemchonga kuwa mchezaji wa safu ya mashambulizi.
Hata hivyo, shuleni na timu ya mtaani ya Nangili FC chini ya Ken Kivaywa alikuwa anawajibishwa nafasi ya beki mkabaji na kiungo mvamizi au straika.
“Niligundua yeye kuwa mchezaji mzuri ambaye anaweza kustahamili mawimbi ya timu pinzani akiwa kikosini na si mchezaji wa kudanadana anaposhika mpira.
Akiwa na boli, huazimia tu kutuma mkwaju langoni kuzua kichefuchefu kinachosababisha ufungaji wa goli kwa timu. Pili, akiwa ndani ya sanduku huwa hana lingine mbali ni kujaribu kusukuma kombora langoni kusababisha kizaazaa.
Tatu, ni mchezaji aliye na uwezo wa kubadilisha gemu akitumia guu lake au kichwa. Kando na kuwa mwiba katika kugonga kiki za ikabu na matuta ambazo huacha makipa hoi,” aeleza mkufunzi huyo ambaye anaamini kwamba mwanasoka huyu akipewa mazingira bora zaidi au jukwaa la kuangazia talanta kupitia udhamini zaidi wa mojawapo ya klabu kuu nchini ambazo zinapiga gozi ya hadhi (Supaligi na Primia), anaweza kufika mbali.
Fauka ya hayo, anafanya juu chini kuendelea kumtafutia timu ambayo itaweza kukitambua zaidi kipaji chake na kumpa fursa ya kucheza,” anasema Kivaywa.
Jitihada zake timuni zimempelekea kuwa mfungaji bora katika ligi ya KFF kisha FKF NWRL ambapo amemimina mabao si haba tangu ajiunge timu.
Baada ya kujiunga na Carpet, mwaka wa 2008 na 2009, aliiwezesha kutamba baada ya kuwa mfungaji bora baada ya kupachika magoli 28 na 21 mtawalia wakicheza ligi ya KFF, Kaunti ya Nairobi na hata kukabidhiwa kiatu cha dhahabu kutoka kwa kocha wake, jambo ambalo lilimtia hamasa ya kuchochea kipaji chake ligini na kuwa na mshawashi zaidi.
Kwa misimu mitatu wakicheza ligi ya Regional (Kanda ya Nairobi) 2011-2012, 2013-2014 na 2015-2016 alicheka na nyavu Mara 14, 15 na 18 mtawalia.
Hata hivyo, baada ya ligi kubadilishwa na kuitwa FKF, NWRL kwa misimu miwili timu imepepetana ligini, alijaza kapuni la timu mwaka jana kwa kufunga magoli 16 ilhali mwaka huu kufikia kuandika kwa makala haya, ametia ndani mabao tisa na kuchangia kufumwa kwa magoli mengine ya timu.
Otiende anasema anaendelea kuimarisha fomu yake kwa kuepukana na mihadarati, kujinoa sawasawa kujenga usuli, kutumia wakati wake vyema na kutizama jinsi wanasoka wengine wanavyocheza kwani anaamini kujijenga kuna hitaji juhudi za mikono yote miwili.
Otiende angependa kuvalia jezi ya AFC Leopards. Mchezaji Jacques Tuyisenge wa Gor Mahia ndiye kivutio chake pamoja na mshambulizi wa Arsenal Pierre Emerick Aubameyang.
Mwanasoka huyo amerithi pia talanta kutoka kwa wajomba zake Antony Obaye na Micah Obaye.
Anasema anastahamili kucheza kama straika kwa kukula lishe bora na kujiepusha na mihadarati.
Wito wake kwa wachezaji ni kwamba, waasi kiburi, wawe na nidhamu na wawe radhi kuelekezwa wabobezi na wakufunzi wa kabumbu wakijua kwamba soka ni fumbo kubwa kwa wachezao.