Michezo

Pep Guardiola asema Manchester City watawaandalia Liverpool gwaride la heshima

June 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Pep Guardiola amethibitisha kwamba wanasoka wake wa Manchester City watawaandalia Liverpool gwaride la heshima watakaposhuka dimbani kwa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Julai 2, 2020.

Mchuano huo utakuwa wa kwanza kwa Liverpool tangu wanyanyue ubingwa wa taji la EPL msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha miaka 30.

Masogora hao wa kocha Jurgen Klopp walithibitishiwa ufalme huo baada ya Chelsea kuwapepeta Man-City 2-1 katika gozi la EPL lililowakutanisha uwanjani Stamford Bridge mnamo Alhamisi ya Juni 25, 2020.

“Tutawaandalia gwaride la heshima bila shaka. Tutawapokea na kuwasalimu Liverpool kwa njia spesheli watakapokuja nyumbani kwetu. Tutawapa heshima hizo kwa sababu kusema kweli, wanastahili,” akasema Guardiola.

Alipoulizwa iwapo atarefusha mkataba wake uwanjani Etihad baada ya ule wa sasa kutamatika mnamo 2021, Guardiola alikataa kujibu.

Kufikia wakati huo, Guardiola atakuwa amehudumu kambini mwa Man-City kwa misimu mitano, kipindi hicho kikiwa kirefu zaidi kuliko kile alichotumia kudhibiti mikoba ya Barcelona nchini Uhispania.

Kocha huyo wa zamani wa Bayern Munich anahusishwa pia na uwezekano mkubwa wa kuyoyomea Italia kuwanoa masogora wa Juventus ambao kwa sasa wanatiwa makali na mkufunzi wa zamani wa Chelsea, Maurizio Sarri.

Akizungumza kabla ya kuwaongoza Man-City kuvaana na Newcastle United katika robo-fainali ya Kombe la FA uwanjani St James’ Park hapo jana, Guardiola alisema kwamba ana kiu ya kukamilisha msimu huu kwa matao ya juu na ikiwezekana kutwaa Kombe la FA na taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

“Matamanio yangu ni kwa sasa ni kuongoza Man-City kutia fora katika mashindano yaliyosalia muhula huu ili kupata hamasa ya kutamba hata zaidi msimu ujao. Tutaona kitakachofanyika baada ya hapo. Sitaki kufikiria sana kuhusu vitu vya misimu miwili ijayo,” akaongeza.