Peres Jepchirchir aunga orodha ya mwisho ya wawaniaji wa tuzo ya Mwanariadha Bora wa Mwaka Duniani 2020
Na CHRIS ADUNGO
BINGWA wa dunia wa mbio za nusu marathon, Peres Jepchirchir ametinga orodha ya wawaniaji watano wa mwisho wa taji la Mwanariadha Bora wa Mwaka 2020 Duniani kwa Wanawake.
Washindi wa tuzo hiyo kwa upande wa wanaume na wanawake watatangazwa rasmi mnamo Disemba 5, 2020 kupitia njia ya mtandao.
Faith Chepng’etich na Hellen Obiri waliokuwa Wakenya wengine kwenye orodha ya awali ya wanariadha 10 walioteuliwa kuwania tuzo hiyo walitemwa.
“Licha ya changamoto tele zilizotokana na janga la corona mwaka huu, wanariadha hao watano ambao wanawakilisha mataifa matano na maeneo manne wanachama wa Shirikisho la Riadha Duniani (WA), waliridhisha sana katika vitengo walivyovishiriki mwaka huu,” ikasema sehemu ya taarifa ya WA.
Jepchirchir alifaulu kutetea ubingwa wa taji la Nusu Marathon ya Dunia jijini Gdynia, Poland mnamo Oktoba 17, 2020. Muda wa saa 1:05:16 alioutumia kukamilisha mbio hizo ulimshuhudia akiimarisha rekodi yake ya nusu marathon kwa wanawake pekee kwa muda wa sekunde 18 chini ya kipindi cha wiki sita.
Mnamo Septemba 5, 2020, mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 27 aliyeibuka bingwa wa Nusu Marathon ya Dunia kwa mara nyingine mnamo 2016, alikuwa amevunja rekodi kwa mpya wa saa 1:05:34 jijini Prague, Jamhuri ya Czech.
Jepchirchir kwa sasa atatoana jasho na Mwethiopia Letesenbet Gidey aliyeweka rekodi ya dunia ya dakika 14:06.62 kwenye mbio za mita 5,000 na Mholanzi Sifan Hassan aliyeweka rekodi ya dunia kwa kukimbia umbali wa kilomita 18.930 chini ya kipindi cha saa moja mnamo 2020.
Wawaniaji wengine wa taji hilo ni Elaine Thompson-Herah na Yulimar Rojas wa Venezuela ambaye hakushindwa katika mapambano manne ya ukumbini na uwanjani katika fani ya kuruka mara tatu. Nyota huyo alivunja rekodi ya dunia kwenye fani ya ukumbini ya kuruka mara tatu (mita 15.43).
Thompson-Herah hakushindwa katika mapambano saba ya mbio za mita 100 ambazo zilimshuhudia akikamilisha kila mojawapo ya mbio hizo chini ya kipindi cha sekunde 10.85.
Bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500, Mkenya Timothy Cheruiyot hakutiwa kwenye orodha ya watimkaji watano wa mwisho watakaowania taji la Mwanariadha Bora wa Mwaka Duniani kwa upande wa wanaume mwaka huu wa 2020. Kudondoshwa kwa Cheruiyot kunamsaza Joshua Cheptegei wa Uganda akiwa miongoni mwa wawaniaji watatu wanaopigiwa upatu zaidi kati ya watano kwenye orodha ya mwisho.
Cheptegei alivunja rekodi za dunia kwenye mbio za mita 5000 (12:35.36), mita 10,000m (26:11.00) na kilomita tano (5km) barabarani kwa muda wa dakika 12:51.
Akishiriki mbio za Nusu Marathon za Dunia kwa mara ya kwanza, Cheptegei aliambulia nafasi ya nne nchini Poland mnamo Oktoba 17, 2020.
Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) limeteuliwa pia kuwania taji la Shirikisho Bora mwanachama wa WA almaarufu Member Federation Award kwa ufanisi wa kuandaa mbio za Kip Keino Classic mnamo Oktoba 3, 2020.
Riadha hizo zilikokuwa sehemu ya mbio za Dunia za Mabara (World Athletics Continental Tour) zilifanyika katika uwanja wa Nyayo, Nairobi.
AK itashindana na mashirikisho matano mengine wanachama wa WA kwenye tuzo hizo ambapo mshindi atatangazwa rasmi mitandaoni mnamo Disemba 5.
Licha ya changamoto tele za kifedha zilizochangiwa na janga la corona, Wakenya walijituma katika mbio za Kip Keino Classic zilizohudhuriwa na mashabiki 6,000. Mbio hizo zilivutia zaidi ya wanariadha 150 kutoka mataifa 30 tofauti.
Kati ya Wakenya waliotamba katika mbio hizo ni mabingwa wa dunia Obiri, Cheruiyot na Beatrice Chepkoech waliotawala vitengo vyao vya mita 5,000, mita 1,500 na mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji mtawalia.
Mbali na AK, wawaniaji wengine wa tuzo hiyo ya kimataifa ni mashirikisho ya riadha nchini New Zealand, Nicaragua, Poland, Peru na Palestine.