Michezo

PESA KWANZA: United yatoa onyo kuhusu uhamisho

June 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United imetuma onyo kali kwa klabu zinazomezea mate kiungo wake nyota Paul Pogba baada ya kuzitangazia haitaharibu wakati kuzisikiza zisipoweka Sh19.2 bilioni mezani, tetesi zinasema.

Bei hiyo huenda inalenga miamba wa Uhispania Real Madrid na wafalme wa Italia Juventus ambao nyota huyu amekuwa akiwakosesha usingizi wakiwaza jinsi ya kupata huduma zake.

Aidha, Manchester United inalenga ‘kupindua serikali’ dakika ya mwisho kuhusu uhamisho wa Antoine Griezmann anayeaminika kuwa mbioni kutua Barcelona kutoka Atletico Madrid.

‘Mashetani wekundu’ United wako tayari kuvunja rekodi yao sokoni kwa kutangazia Atletico ofa ya Sh12.2 bilioni ili kupata mshambuliaji huyu Mfaransa.

Barca ilionekana kuwa pua na mdomo kunyakua mshindi huyu wa Kombe la Dunia, lakini kujikokota kwake kumvizia rasmi kumefungulia United mlango.

Na, viongozi wa United huenda sasa wakamrukia wanapojiandaa kutengana na mshambuliaji Mbelgiji Romelu Lukaku na kiungo Mfaransa Paul Pogba aliyegharimu klabu hiyo Sh11.4 bilioni kutoka Juventus.

Griezmann, 28, aliipa United matumaini tele alipodai kwamba maisha yake kama msakataji wa kabumbu huenda sasa yatakuwa nje ya Uhispania.

Akizungumza Jumanne baada ya Ufaransa kupapura Andorra 4-0 katika mechi yake ya kufuzu kushiriki Kombe la Bara Ulaya (Euro) 2020, alisema, “Sijui kama nitasalia katika La Liga.

“Najua ninakotaka kuenda. Pia mimi niko na hamu kubwa ya kuona uhamisho huu unakamilika haraka iwezekanavyo.”

Griezmann alikasirisha waajiri wake Atletico mwezi Mei alipotangaza kwamba anapanga kujiunga na Barca katika kipindi hiki kirefu cha uhamisho.

Neymar Jr

Hata hivyo, alijipata akining’inia baada ya miamba hao wa Uhispania kuanza kutamani mchezaji wao wa zamani Neymar, ambaye ni mali ya Paris Saint-Germain.

Tamaa ya Barca kwa Neymar imeipa United motisha, ingawa inafahamu fika kwamba kukosa kumpa Griezmann burudani la Klabu Bingwa Ulaya msimu 2019-2020 ni tatizo kubwa.

Hata hivyo, fununu zinasema kuwa mabingwa hawa mara 20 wa Uingereza wako tayari kulipa ada hiyo pamoja na mshahara wa kutisha wa Sh57.8 milioni kila wiki.

Mabwanyenye PSG wana hamu kubwa ya kurejesha mshambuliaji huyu nyumbani nchini Ufaransa. Hii inaweka presha kwa United itakayohitajika kutafuta njia ya kushawishi Griezmann kuwa anafaa kuongoza mabadiliko makubwa uwanjani Old Trafford chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Habari zaidi kutoka Old Trafford zinasema kwamba United imeamua kumpa kisogo winga matata wa Madrid, Gareth Bale.

Raia huyu wa Wales yuko sokoni katika kipindi hiki kirefu cha uhamisho wakati Real inalenga kutafuta kuchangisha fedha ili kugharimia mabadiliko makubwa chini ya kocha Zinedine Zidane.

Hata hivyo, United imekataa fursa ya kuzungumza na Real kuhusu kuajiri Bale kabisa ama kwa mkopo.

Ed Woodward amekuwa akilenga Bale katika kila kipindi kirefu cha uhamisho tangu achukue majukumu ya kuajiri uwanjani Old Trafford mwaka 2013.

Naibu huyu mwenyekiti ametupilia mbali ndoto hiyo aliyoshikilia kwa muda mrefu ya kusajili mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 29 na kuamua kuunga kocha Ole Gunnar Solskjaer katika juhudi zake za kuajiri talanta changa nchini Uingereza.