Michezo

Pigo Inter Milan jeraha likimweka nje Lukaku katika mechi ya UEFA dhidi ya Real Madrid

November 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI nyota Romelu Lukaku, 27, hatakuwa katika kikosi kitakachotegemewa na kocha Antonio Conte wa Inter Milan katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya miamba wa Uhispania, Real Madrid inayochezwa leo Jumanne usiku.

Hii ni baada ya nyota huyo wa zamani wa Manchester United kupata jeraha la paja.

Lukaku ambaye ni raia wa Ubelgiji amefungia waajiri wake mabao saba hadi kufikia sasa msimu huu.

Inter kwa ssa wanashikilia nafasi ya pili kwenye Kundi B la UEFA baada ya kujizolea alama mbili pekee kutokana na michuano miwili iliyopita. Lukaku alichangia mojawapo ya pointi hizo zinazojivuniwa na Inter baada ya kuwaongoza waajiri wake kusajili sare ya 2-2 dhidi ya Borussia Monchengladbach ya Ujerumani.

Katika kampeni za msimu uliopita wa 2019-20, Lukaku alipachika wavuni mabao saba na kusaidia Inter kukamilisha kampeni za Europa League katika nafasi ya pili nyuma ya Sevilla ya Uhispania.

Kukosekana kwa Lukaku katika kikosi cha Inter dhidi ya Real kunatarajiwa kumpisha fowadi wa zamani wa Arsenal na Man-United, Alexis Sanchez ambaye amepona jeraha baada ya kukosa mechi tatu zilizopita.

Kwa upande wao, Real ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha Zinedine Zidane watakosa maarifa ya wachezaji Eder Militao, Nacho Fernandez, Dani Carvajal na Martin Odegaard.

Real kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) baada ya kupoteza mchuano mmoja pekee. Wako nyuma ya Real Sociedad iliyo na alama 17 ikiwa ni moja mbele ya Real Madrid. Ingawa hivyo, fomu yao imekuwa mbovu kwenye UEFA huku wakijizolea alama moja pekee kutokana na mechi mbili zilizopita.

Masogora wa Zidane walihitaji mabao mawili ya dakika za mwisho katika sare ya 2-2 dhidi ya M’gladbach ambao kwa sasa wanakokota nanga mkiani mwa Kundi B.