Michezo

Pigo kwa KPL Uhuru akirefusha marufuku

June 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MIPANGO ya vinara wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kukamilisha kampeni za kipute hicho msimu huu imekabiliwa na pigo jingine baada ya serikali kuongeza muda wa marufuku ya mikusanyiko ya umma kwa mwezi mmoja zaidi.

Katika hotuba yake kwa taifa mnamo Juni 6, 2020, Rais Uhuru Kenyatta alisisitiza kwamba maamuzi hayo ya kutolegeza kabisa baadhi ya kanuni za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 yalikuwa zao la mashauriano ya kina na wataalamu wa afya.

KPL ambao ni waendeshaji wa Ligi Kuu ya humu nchini wanapania kupigisha abautani maamuzi ya awali ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) ya kutamatisha kipute cha msimu huu bila ya kushauriana nao. Hadi hatua hiyo ilipochukuliwa na FKF, zilikuwa zimesalia mechi tisa zaidi za kusakatwa.

Kamati Kuu ya KPL inatarajiwa kukutana wiki hii kujadili uwezekano wa kurejelewa kwa kampeni za muhula huu kuanzia Septemba 2020.

Mbali na kanuni mpya za serikali, matumaini ya KPL katika kufaulu kwa maazimio yao yamedidimizwa zaidi na hatua ya Jopo la Mizozo ya Spoti (SDT) kuahirisha maamuzi ya kesi kati ya KPL na FKF.

Kwa upande wake, Nick Mwendwa ambaye ni Rais wa FKF ameshikilia kwamba klabu za humu nchini hazina uwezo wala miundo-msingi ya kuafikia kanuni za afya katika mwongozo mpya uliotolewa majuzi na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Kwa mujibu wa Mwendwa ambaye anawania fursa ya kuhifadhi wadhifa wake katika FKF, hali ngumu ya kifedha inayokabili vikosi vyote vya KPL kwa sasa itatatiza juhudi za kufanikisha maandalizi ya mapambano hayo.

Waziri wa Michezo, Amina Mohammed ametangaza kuwa kamati maalumu itaundwa wiki hii ili kutathmini mipangilio ya michezo mbalimbali kurejea kwa kuzingatia kanuni na sheria zilizowekwa na Wizara ya Afya.

Wakati uo huo, mwenyekiti wa Kariobangi Sharks, Robert Maoga ametaka FKF kufutilia mbali kivumbi cha Shield Cup msimu huu.

Kabla ya shughuli zote za michezo kusitishwa humu nchini mnamo Machi 2020, kivumbi cha Shield Cup ambacho humpa mshindi fursa ya kuwakilisha Kenya kwenye Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup), kilikuwa kimefikia hatua ya 16-bora.

Wito umetolewa na wadau mbalimbali kukubalia Bandari ambao ni mabingwa watetezi wa Shield Cup kunogesha kampeni za CAF Confederations Cup muhula ujao.

FKF tayari imewasilisha jina la Gor Mahia kwa vinara wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ili wawakilishe Kenya kwenye kivumbi cha Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) muhula ujao.