PIGO KWA MAN-U: Pigo kuu Trafford, Rashford kukaa nje miezi 2
Na MASHIRIKA
MERSEYSIDE, Uingereza
SAA chache baada ya kulazwa mabao 2-0 na Liverpool, masaibu ya Manchester United yaliongezeka kufuatia ripoti kwamba mshambuliaji Marcus Rashford atakaa nje bila kucheza kwa kati ya miezi miwili na miezi mitatu.
Kocha Ole Gunnar Solskjaer ametaarifu kwamba nyota huyo anaendelea kusumbuliwa na jeraha la mgongoni alilopata hapo awali wakicheza na Wolves katika pambano la FA Cup.
Kadhalika jeraha hilo ni pigo kuu kwa kocha Gareth Southgate wa timu ya taifa ya Uingereza ambayo inajiandaa kushiriki fainali za Kombe la Euro 2020 mwezi Juni.
Kuumia kwake kumetokea siku chache tu baada ya nahodha wa timu hiyo, Harry Kane kuumia mguuni, ambapo huenda akakaa nje hadi msimu umalizike.
Kulingana na kocha wa klabu yake ya Tottenham Hotspur, Kane atakuwa nje hadi katikati ya mwezi Aprili, ambapo atazikosa mechi mbili za kipimana nguvu dhidi ya Italia na baadaye Denmark.
Kabla ya kukabiliana na Liverpool, Solskjaer alisema Rashford alikuwa na majeraha mawili tofauti, moja likiwa limemsumbua kwa muda mrefu.
Alisema jeraha hilo lilizidi baada ya kuchezewa ngware na Matt Doherty wa Wolves, Jumatano iliyopita.
“Kumbukeni kulikuwa na hali kama hii ambapo ilibidi Anthony Martial akae nje kwa wiki nane, ikabidi tuanze kumchezesha Mason Greenwood. Itabidi tufanya hivyo kwa mara nyingine.”
United wanapanga kusajili wachezaji kadhaa mwezi huu na tayari wameanza kutambuwa wachezaji kadhaa watakaofikiriwa kwa nafasi hizo.
“Tunajaribu kuzungmza na kiungo Bruno Fernandes, miongoni mwa wengine. Kikosi cha Solskjaer kinakabiliwa na hali ngumu baada ya mastaa kadhaa wakiwemo Paul Pogba na Scott McTominay kuumia.
“Tuna wachezaji watatu muhimu wanauuguza majeraha na awataktaa nje kwa muda mrefu. Huenda tukalazimika kusajili wengine kwa mikataba ya muda mfupi. Lakini leo sitawaambia ni akina nani tunalenga,” kocha aliwaambia waandishi Jumapili baada ya kushindwa na Liverpool.
Mara tu baada ya mechi hiyo kumalizika, kocha Jurgen Klopp wa Liverpool alirejelea maoni yake kwamba taji ni lao.
“Tunpaswa kuanza kusherehekea matokeo mazuri yanayofuatana lakini ligi haijamalizika, ingawa tunatarajia kutawazwa mabingwa mapema,” alisema.
“Kila mtu amecheza vizuri zaidi leo, ikikumbukwa tulikuwa tukicheza na timu kubwa iliyo na wachezaji kadhaa wa vipaji vya hali ya juu.”
Barcelona
Kwingineko, kocha mpya wa Barcelona, Quique Setien alianza jukumu lake kwa kishindo, kufuatia bao lililofungwa na Lionel Messi zikibakia dakika 15 mechi kumalizika.
Baada ya kuutawala mchezo huo dhidi ya Granada kwa asilimiA kubwa bila kufunga bao, Messi alishirikiana vyema na Antoine Griezmann pamoja na Arturo Vidal kabla ya kupachika wavuni bao hilo muhimu.
Kabla ya mechi hiyo, Setien alikuwa ameahidi mashabiki soka ya kupendeza, mbali na ushindi.
Kufuatia matokeo hayo, Barcelona imerukia kilele cha La Liga.