• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Pigo kwa Simbas msimu wa raga ukifutwa

Pigo kwa Simbas msimu wa raga ukifutwa

Na CHRIS ADUNGO

KIPUTE cha raga cha Barthes Cup kilichokuwa kimeratibiwa upya kuandaliwa humu nchini mnamo Septemba 2020 sasa hakitafanyika.

Hii ni baada ya Shirikisho la Raga la Afrika kufutilia mbali kampeni zote za msimu huu kufuatia ushauri wa vinara wa mashirikisho wanachama waa Raga ya Afrika na maafisa wa afya kuhusu hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 duniani.

Yalikuwa matumaini ya Shirikisho la Raga la Afrika kushuhudia mapambano mbalimbali yakirejelewa mwezi ujao lakini hilo halitawezekana kwa kuwa janga la corona bado halijadhibitiwa vilivyo.

Ina maana kwamba kampeni za kuwania ubingwa wa Africa Cup hazitafanyika kwa mwaka wa pili mfululizo. Mwaka jana, kivumbi hicho hakikuandaliwa kutokana na uchechefu wa fedha.

Aidha, mapambano ya raga ya wachezaji saba kila upande kwa wanaume na wanawake pamoja na Barthes Cup ambayo hushirikisha wanaraga chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, hayatanogeshwa. Hata hivyo, nchi zilizokuwa zishiriki vipute hivyo zitakubaliwa kuvaana kirafiki iwapo hali itakuwa nafuu baadaye mwaka huu.

Kocha Paul Odera wa timu ya taifa ya wanaraga 15 kila upande almaarufu Simbas na kikosi cha U-20, amesema maamuzi hayo ni pigo kubwa kwa kikosi chake ambacho sasa hakitashiriki mapambano yoyote ya haiba kubwa mwaka huu. Isitoshe, matumaini yao ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2023 sasa yamedidimizwa zaidi.

“Yasikitisha kwamba tutakuwa na mwaka mmoja pekee wa kujiandaa kwa mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia. Hili ni jambo linalotuweka katika hali ngumu zaidi,” akasema.

Simbas kwa hivyo, watakosa fursa ya kuvaana na miamba wa raga ya Afrika, Namibia kwa mwaka wa pili mfululizo.

“Mataifa yote hayatalegeza masharti yaliyowawekea raia wao kwa wakati mmoja. Kuendelea na mapambano haya kutakwaza baadhi ya nchi zinazoshiriki. Aidha, gharama ya usafiri itakuwa ya juu na huenda baadhi ya timu zikalazimika kuwekwa karantini,” ikasema sehemu ya taarifa ya Shirikisho la Raga la Afrika.

Mechi za Simbas zilitarajiwa kuanza Juni 13 kwa pambano dhidi ya Morocco jijini Mombasa. Mchuano wa pili ungaliwashuhudia wakisafiri jijini Abidjan, Ivory Coast mnamo Juni 27. Waliratibiwa baadaye kuvaana na Uganda kwenye nusu-fainali za Victoria Cup mjini Kakamega mnamo Julai 11 kabla ya kuwaalika Zimbabwe mnamo Julai 18 mjini Nakuru.

Katika makala ya Raga ya Afrika mwaka jana, Simbas waliambulia nafasi ya pili nyuma ya Namibia barani kabla ya kupepetwa na Canada, Hong Kong na Ujerumani katika kundi la kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Kenya ilitazamia kutumia mashindano ya Barthes Cup kufuzu kwa Raga ya Dunia kwa Chipukizi (JWRT) nchini Uhispania mnamo Disemba 2020 na kipute cha Africa Cup kujikatia tiketi ya fainali Kombe la Dunia nchini Ufaransa mnamo 2023.

You can share this post!

Fainali za handiboli ni hapo mwakani

Kakamega High kujenga uwanja wa Sh120 milioni

adminleo