Pigo Manchester City Aguero akirudi tena mkekani baada ya kupata jeraha la goti
Na MASHIRIKA
FOWADI Sergio Aguero wa Manchester City atalazimika tena kusalia mkekani kwa kipind kirefu baada ya kupata jeraha la misuli ya miguu kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowashuhudia wakisajili sare ya 1-1 dhidi ya West Ham United mnamo Oktoba 24 uwanjani London Stadium.
Aguero, 32, alirejea uwanjani kusakata boli mnamo Oktoba 17, 2020 dhidi ya Arsenal baada ya kuwa nje kwa takriban miezi minne akiuguza jeraha la goti.
Jeraha la Aguero ni pigo kubwa kwa Man-City ambao tayari wanatarajiwa kukosa huduma za mshambuliaji Gabriel Jesus na mabeki Aymeric Laporte na Nathan Ake.
Baada ya kuambulia sare dhidi ya West Ham, Man-City kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Olympique Marseille ya Ufaransa kwenye Klabu Bingwa Ulaya kabla ya kurejelea kampeni za EPL dhidi ya Sheffield United.
Akicheza dhidi ya Arsenal mnamo Oktoba 17, Aguero aliwajibishwa kwa kipindi cha dakika 65 pekee na akafunga bao lake la 40 kwenye kivumbi cha UEFA dhidi ya FC Porto mnamo Oktoba 21, 2020. Fowadi huyo raia wa Argentina alichezeshwa kwa dakika 68 kwenye mechi hiyo dhidi ya Porto ambayo Man-City walisajili ushindi wa 3-1 uwanjani Etihad.
Guardiola anahofia kwamba wingi wa visa vya majeraha kambini mwake ni huenda ukazamisha kabisa matumaini ya kikosi chake kutwaa ubingwa wa EPL au UEFA msimu huu.
Guardiola amesema kiini cha kusajiliwa kwa Ruben Dias ni haja ya kuziba pengo la aliyekuwa nahodha wao Vincent Kompany aliyejiunga na Anderlecht ya Ubelgiji mwishoni mwa msimu wa 2018-19.
Kwa mujibu wa Guardiola, kushindwa kwa Man-City kupata kizibo cha Kompany msimu uliopita wa 2019-20 kulichangia utepetevu wa kikosi chake kilichokosa kutoa ushindani uliotarajiwa kwa Liverpool ambao hatimaye walitawazwa mabingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.
“Yasikitisha kwamba tunaziba pengo moja na mengine kupatikana. Tunasubiri tathmini ya madktari ili tujue kipindi cha muda ambacho Aguero atakuwa nje,” akasema Guardiola ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich.
Jesus atakuwa nje kwa majuma matatu kuuguza jeraha la mguu alilolipata katika mechi ya EPL iliyowakutanisha na Wolves uwanjani Molineux mnamo Septemba 21.
“Kuumia kwa Jesus na Aguero, kisha Ake na Laporte ni balaa. Hili ni tukio ambalo linatishia kutuzamisha kabisa japo tunatumainia kwamba mambo yatakuwa shwari,” akaongeza mkufunzi huyo raia wa Uhispania.
Kukosekana kwa Jesus na Aguero kunatarajiwa kumpa nafasi chipukizi Liam Delap kushirikiana na Raheem Sterling na Phil Foden kwenye safu ya mbele ya Man-City.