Michezo

Pogba haendi popote, Ole Gunnar asema

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United amekutana na kiungo Paul Pogba ambaye ameonyesha dalili za kuendelea kuichezea klabu hiyo ya Old Trafford.

Solskjaer ametoa ripoti hii muda mfupi tu baada ya kocha Zinedine Zidane wa Real Madrid ya Uhispania kusema anammezea mate Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 26.

“Pogba anajua kufanya kila kitu uwanjani. Anatoa mchango mkubwa kikosini na ni wachezaji wachache wanaoweza kukifanya anachokifanya yeye binafsi,” Zidane aliwaambia waandishi mwishoni mwa wiki.

Pogba amekuwa akisemekana kuwa anataka kuhamia katika klabu hiyo ya Bernabeu na aliwahi kueleza Real Madrid kama ‘timu ya ndoto yake’ alipokuwa akichezea timu ya taifa ya Ufaransa.

“Ni jukumu langu kuzumgumza na wachezaji wangu wakati wowote, wala sikusema naye kwa sababu anavutia Zidane. Nimezungmza naye moja kwa moja na tumeelewana,” aliongeza kocha huyo.

“Atazidi kuzidisha bidii yake hapa kwa sababu anaelewa uhusiano wangu naye ni mzuri. Paul ni mchezaji mzuri wa kati ya ushambulizi anayeelewa jinsi ya kuzuia na namna ya kushambulia. Nampenda kutokana na ushawishi wake kikosini. Kila mtu anamfurahia hapa klabuni.”

Pogba alijiunga tena na United kutoka Juventus ambapo alivunja rekodi ya dunia ya mwanasoka anayelipwa vizuri zaidi, lakini hatma yake pale Old Trafford ilionekana kuwa na utata mapema msimu huu kufuatia malumbano baina yake na kocha Jose Mourinho aliyeondoka Desemba.

Paul Pogba. Picha/ Maktaba

Wakati huo huo, United wanapanga kuteua mkurugenzi wa kiufundi kabla ya msimu huu kumalizika, jambo ambalo tayari Solskjaer amelikubali.

“Soka imebadilika na lazima kuwe na watu wa kutosha, kila mmoja akifanya kazi yake kitaaluma,” alisema kocha huyo mwenye umri wa miaka 46.

Kocha aliyeondoka (Mourinho) alipinga vikali kusajiliwa kwa mkurugenzi wa kiufundi kufanya naye kazi, lakini Solskjaer amekubali pendekezo hilo.

“Miye na Ed (Woodward, naibu mkurugenzi mkuu wa klabu hii) pamoja na mwenzake Joe Glazer, kwa mijanili ya kuimarisha klabu hii tunatafuta njia zozote zinazoweza kuirejesha klabu hii mahali inapostahili.

“Nafurahia kuwa hapa kwa sababu ninashirikiana na watu wanaoelewa soka vyema. Soka inapaswa kuendeshwa vivyo hivyo. Kocha pekee hawezi kuleta ufanisi jinsi alivyofanya Sir Alex Ferguson kuanzia 1986. Nadhania siku hizi soka inahitaji watu wa kutosha kwenye idara ya kiufundi.”

Ujuzi na tajriba

Mkurugenzi wa kiufundi atakayeteuliwa na United lazima awe na ujuzi wa miaka mingi katika kuandaa wanasoka katika vituo vya kunoa vipaji ambaye kazi yake itakuwa pamoja na kutafutia klabu hiyo wachezaji wa kusajiliwa.

Kutoelewana kwa usimamizi na Mourinho uliikosesha United kuwanasa mabeki Harry Maguire wa Leicester City na Jerome Boateng wa Bayern Munich.

Baada ya kucheza na Wolves, United watakutana na West Ham United (nyumbani), Everton (ugenini), Manchester City na Chelsea (nyumbani), Huddersfield Town (ugenini) na Cardiff City (nyumbani).