Pogba injini ya Man United
Na CHRIS ADUNGO
PAUL Labile Pogba, 25, ni kiungo matata mzaliwa wa Ufaransa ambaye kwa sasa anavalia jezi za Manchester United nchini Uingereza.
Japo makocha wake humwajibisha pakubwa kama kiungo mpakuaji, Pogba pia ana uwezo wa kutandaza boli akiwa kiungo mvamizi au kiungo mkabaji.
Akiwa mzawa wa eneo la Lagny-Sur-Marne nchini Ufaransa, Pogba alisajiliwa na Le Harve katika Ligi Kuu ya Ufaransa baada ya kudhihirisha ushawishi mkubwa uwanjani. Baadaye, huduma zake ziliwaniwa na Manchester United waliomsajili mnamo 2009.
Baada ya kukosa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Man-United miaka miwili baadaye, pogba alitua Italia kuvalia jezi za Juventus bila ada yoyote mnamo 2012.
Akipiga soka ya kulipwa nchini Italia, Pogba aliwanyanyulia waajiri wake mataji manne mfululizo ya Serie A, makombe mawili ya Coppa Italia na mengine mawili ya Supercoppa Italiana.
Ushawishi wake ugani ulimfanya kuwa miongoni mwa chipukizi waliostahiwa pakubwa duniani kiasi cha kutuzwa Chipukizi Bora wa Mwaka mnamo 2013 na 2014.
Alijumuisha na UEFA katika Kikosi Bora cha Mwaka mnamo 2015 baada ya kuwachochea Juventus kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya miaka 12.
Ubora wa matokeo ya Pogba kambini mwa Juventus ulimfungulia milango ya kurejea Man-United mnamo 2016 kwa kima cha Sh12 bilioni, fedha zilizomfanya kuwa mchezaji ghali zaidi katika historia ya soka ya Uingereza.
Katika msimu wake wa kwanza uwanjani Old Trafford, Pogba aliwashindia Man-United taji la League Cup na Ligi ya Uropa.
Katika kiwango cha kimataifa, Pogba alivalia utepe wa unahodha wa Ufaransa katika fainali za Kombe la Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, kivumbi kilichomshuhudia akitawazwa Mchezaji Bora mwishowe.
Mwaka mmoja baadaye, alipangwa katika kikosi cha kwanza na kujipa uhakika wa kuwa sehemu ya timu hiyo katika fainali za Kombe la Dunia mnamo 2014.
Utajiri wa kipaji chake ulidhihirika zaidi kwenye fainali za Euro 2016 zilizoandaliwa na Ufaransa. Baada ya kuwasaidia wenyeji hao kuambulia nafasi ya pili nyuma ya Ureno, Pogba aliwaongoza Ufaransa kunyanyua ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Urusi mnamo 2018.
Pogba ambaye ni Mwisilamu, alilelewa na wazazi wake wazaliwa wa Guinea katika eneo la Seine-et-Marne, Ufaransa. Ana kaka wawili pacha – Florentin na Mathias ambao kwa sasa huchezea timu ya taifa ya Guinea.
Florentin kwa sasa huvalia jezi za Genclerbirligi nchini Uturuki huku Mathias akiwawajibikia Tours kutoka Ufaransa.
Nyota huyo ambaye alikuwa shabiki sugu wa Arsenal utotoni mwake, alijitosa katika ulingo wa soka kwa kuvalia jezi za US Roissy-en-Brie akiwa na umri wa miaka sita pekee.
Alikichezea kikosi hicho kwa misimu saba kabla ya kujiunga na US Torcy alikopokezwa utepe wa unahodha wa kikosi cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 13.
Baada ya msimu mmoja na Torcy, maarifa ya Pogba yalihemewa pakubwa na Le Harve waliomteua kuwa nahodha wa kikosi cha U-16 katika msimu wake wa pili.
Chini ya unahodha wake, Le Harve waliambulia nafasi ya pili nyuma ya Lens waliowapiku pia Olympique Lyon na Nancy ligini.
Pogba ana mkataba wa kibiashara na kampuni ya Adidas ambayo ameifanyia mauzo ya nyingi za bidhaa zake kwa ushirikiano na David Beckham, Lionel Messi, Mohamed Salah na mwanamuziki mzawa wa Amerika, Pharrell Williams.
Pogba alianza mwaka huu kwa kuingia katika kikoa cha majanadume kamili baada ya mchumba wake Maria Salaues, 25, kumzalia mtoto.
Nyota huyo alianza kutoka kimapenzi na Maria mnamo Oktoba 2017 baada ya kutemana na Dencia, kichuna ambaye ni mwanamitindo na mfanyabiashara maarufu mzawa wa Cameroon.
Dencia alibanduka katika chaka la mapenzi ya Pogba baada ya starehe zake na sogora huyo kugeuka kero kwa majirani waliokuwa wakiishi nao katika hoteli ya Lowry mwanzoni mwa Novemba 2016.
Wawili hao waliwaweka majirani zao katika ulazima wa kukesha wakisikiliza vilio vibovu vilivyokuwa vikitolewa na Dencia kila mara alipokuwa akishiriki miereka ya chumbani na dume lake.
Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, ilikuwa mazoea kwa kelele zisizokuwa za kawaida kusikika chumbani mwa Pogba kila alipokuwa akilitalii buyu la asali la Dencia katika majira ya usiku na alfajiri ya saa tisa na saa kumi.