Polack sasa ataka kunoa Stars
Na CHRIS ADUNGO
KOCHA Steven Polack wa Gor Mahia amefichua maazimio ya kudhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Harambee Stars ambayo kwa sasa inanolewa na mkufunzi wa zamani wa Tusker na Mathare United, Francis Kimanzi.
Fursa adimu ya kutia makali kikosi cha Stars imewahi kuwavutia wakufunzi wa haiba kubwa wa kigeni kama vile Mbelgiji Adel Amrouche, Bobby Williamson (Scotland), Mbelgiji Paul Put, Mfaransa Sebestien Migne na marehemu Reinhardt Fabisch (Ujerumani) miongoni mwa wengine.
Polack ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Gor Mahia, amesema atakuwa mwepesi wa kuikumbatia nafasi ya kuwa kocha wa Stars iwapo fursa hiyo itajitokeza. Kwa mujibu wake, kunoa timu ya taifa huwa azma ya mkufunzi yeyote anayejivunia uzoefu mkubwa katika soka ya kiwango cha klabu.
Kocha huyo mzawa wa Uingereza na raia wa Finland, alianza kuwatia makali masogora wa Gor Mahia mwaka jana baada ya kuhudumu katika Ligi Kuu ya Ghana kwa kipindi kirefu. Katika taaluma yake ya ukufunzi, hajawahi kuwa kocha wa timu ya taifa.
Kikubwa zaidi kinachomwaminisha kwamba atatambisha kikosi cha Stars, ni uelewa wake wa soka ya humu nchini na mafanikio ambayo amewazolea Gor Mahia chini ya kipindi kifupi.
Polack anashikilia kuwa ndoto za kila kocha huwa ni kukiwezesha kikosi chake cha taifa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia na hilo ndilo angelenga zaidi kuliafikia iwapo atapata fursa ya kusimamia Stars. Ingawa hivyo, kubwa zaidi katika matamanio yake kwa sasa ni kuendelea kuboresha Gor Mahia, kuwaongoza mabingwa hao mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya kunyanyua mataji zaidi na kuwaimarisha katika kampeni za soka ya kimataifa.
“Iwapo nafasi ya kuwa kocha wa Stars itajipa au nafasi hiyo ya kazi kutangazwa, sitachelea kuwasilisha ombi langu. Huenda ni mimi nitakayewapeleka Stars kwenye fainali zijazo za Kombe la Dunia. Nimekuwa na azma ya muda mrefu ya kuongoza timu ya taifa kutinga Kombe la Dunia na nina uhakika wa asilimia 100 kwamba hilo litafanyika nikidhibiti mikoba ya mojawapo ya timu za taifa kutoka bara la Afrika,” akasema Polack.
Polack alizaliwa katika eneo la Birmingham, Uingereza na akawajibikia vikosi vingi vya mtaani akiwa difenda kabla ya kuyoyomea Finland alikochezea FC Inter Turku kwa miaka 14. Chini ya unahodha wake, kikosi hicho kilinyanyua ubingwa wa Ligi Kuu mara moja, mataji mawili ya Finnish Cup na moja la League Cup.
Ilikuwa hadi 1998 ambapo Polack aliangika rasmi daluga zake akiwa na umri wa miaka 37. Alipata fursa ya kunoa kikosi cha King Feisal Babes mjini Kumasi, Ghana mnamo 2007 kisha akaajiriwa na kikosi cha Berekum Chelsea FC cha Ligi Kuu ya Ghana. Alihudumu huko kwa miaka miwili kabla ya kurejea Finland kisha kurudi Ghana mnamo 2017 kuwanoa miamba Asante Kotoko.
Anajivunia kuwa kocha wa kwanza kuibuka mshindi mara tatu katika msimu mmoja wa tuzo ya Fidelity Insuarance-SJAK ambayo hutolewa kwa kocha bora wa Ligi Kuu ya Kenya kila mwezi.