Michezo

Police, Tusker wala huu mikononi wa Homeboyz, Talanta mechi za KPL

Na CECIL ODONGO, WYCLIFFE NYABERI May 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBIO za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu (KPL) Jumatano zilichukua mwelekeo hasi baada ya viongozi Kenya Police na nambari mbili Tusker kupoteza mechi zao.

Kenya Police ilipoteza 2-1 dhidi ya Kakamega Homeboyz uga wa Mumias Sports Complex, Kaunti ya Kakamega.

Tusker kwa upande mwingine, waliondoka Dandora wakiwa wameinama vichwa baada ya kutandikwa 2-0 na FC Talanta.

Licha ya kupoteza huko, Kenya Police bado wanaongoza KPL kwa alama 58 kutokana na mechi 31 zikiwa zimesalia mechi tatu msimu huu utamatike.

Kupoteza kwa Tusker kuna maana kuwa bado wapo nambari mbili kwa alama 55 wakiwa wamecheza mechi mbili zaidi kuliko nambari tatu Gor Mahia.

Matokeo hayo ni nafuu kwa Gor Mahia ambao watavaana na Nairobi City Stars Alhamisi katika uga wa Dandora.

Gor wapo nafasi ya tatu kwa alama 53 wakiwa na mechi mbili kibindoni na ushindi dhidi ya Simba wa Nairobi Alhamisi utawaweka hadi nafasi ya pili kwa alama 56.

Uwanjani Dandora, Emmanuel Osoro alifunga bao lake la 15 na 16 na kuwanyima Tusker alama zote tatu kwenye mchuano ambao wanamvinyo hao walihitaji alama zote.

Osoro sasa amefunga mabao sawa na Moses Shumah wa Kakamega Homeboyz wote wakifukuzia Kiatu cha Dhahabu.

Wawili hao wamempita Ryan Ogam ambaye amekuwa akipambana na majeraha na hajafungia klabu tangu Januari 15.

Ogam alifunga mara ya mwisho wakati ambapo Tusker ilipiga Bandari 2-1 uga wa Mbaraki Mombasa na ana mabao 15.

Shumah alifunga bao lake la 16 kwa Homeboyz ambayo bao lake jingine lilifungwa na Glen Otunga. Mohamed Bajaber alifunga bao la kufutia machozi kwa Kenya Police,  hili likiwa bao lake la tisa la msimu.

Tusker, mabingwa mara 13 sasa itawalazimu wapambane kwenye mechi tatu za mwisho dhidi ya Sofapaka, Kariobangi Sharks na Kakamega Homeboyz.

Ubingwa sasa haupo kwenye mikononi mwao na lazima wategemee Kenya Police au Gor Mahia wateleze. Police wamesalia na mechi ngumu dhidi ya FC Talanta, Shabana na Gor Mahia wakilenga kuandikisha historia ya kutwaa ubingwa wa KPL kwa mara ya kwanza.

Katika mechi nyingine, kinda wa Shabana Austin Odongo na Brian Michira walifungia Tore Bobe 2-1  kwenye ushindi dhidi ya Bidco United ugani Gusii.

Kakamega Homeboyz wana alama 51 huku Shabana ikiwa na alama 52 zikiwa zimesalia mechi tatu msimu huu utamatike.

Mara Sugar na Bandari nazo ziliagana sare tasa, Murangá Seal ikachapa Sofapaka 2-0 na kufufua matumaini ya kukwepa kushushwa ngazi.

AFC Leopards walipata mteremko Kayci Odhiambo, Ronald Sichenje na Christopher Koloti wakiwafungia dhidi ya Mathare United. Vijana hao wa mtaa wa mabanda walipata bao la kufuta machozi kupitia John Nyawir.