• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Presha kwa Arsenal ikihitaji pointi 2 kumaliza EPL katika nafasi ya 2

Presha kwa Arsenal ikihitaji pointi 2 kumaliza EPL katika nafasi ya 2

Na MWANGI MUIRURI

KLABU ya Arsenal inahitaji pointi mbili pekee katika mechi zake mbili ilizosalia nazo katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ili itawazwe kuwa ya pili, ikiwa ubingwa utaiponyoka.

Arsenal kwa sasa ikisalia na mechi mbili pekee ni ya kwanza katika jedwali ikiwa na pointi 83 lakini Liverpool iliyo ya tatu kwa pointi 75 ikiwa na uwezo wa kumaliza ikiwa na pointi 84 kutokana na mechi tatu iliyosalia nazo.

Hali hii inaitia Arsenal presha ya kujidhibiti ili angalau kikiumana, imalize ya pili.

Huenda ijipate taabani iwapo itakung’utwa na Manchester United ambayo inawangojea ugani Old Trafford mnamo Mei 12, 2024.

Mechi ya mwisho kwa Arsenal ni dhidi ya Everton, timu ambayo huwa haieleweki kabisa kwa kuwa huwa na uwezo wa kushinda, kushindwa na kutoka sare kwa raha zake.

Everton licha ya kupokonywa pointi sita kwa kukiuka maadili ya kibiashara katika EPL, imepambana na kuishia kuhepa shoka baada ya kujidhibiti hadi sasa katika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 36.

Mwanzoni ilikuwa imepokonywa pointi 10 kabla ya rufaa iliyokata kuipa afueni.

Hali hiyo inafanya mechi hizo mbili za Arsenal kuwa hatari na ikizipoteza huku nayo Liverpool ifanye mambo katika zake tatu, basi Arsenal itajipata ikimaliza katika nafasi ya tatu.

“Afueni kwa Arsenal ni ishinde mechi zake zote ndio itegee kama kuna bahati ya mkosi kwa Man City ambayo kwa sasa iko katika nafasi ya pili kwa pointi 82 lakini ikiwa na mechi tatu ambazo haijacheza ambapo ikiibuka mshindi kwa zote itaishia kuwa mabingwa kwa pointi 91 huku uwezo wote wa Arsenal ukiwa ni kumaliza kwa pointi 89,” asema Diblo Kaberia, mchanganuzi wa masuala ya soka.

Kaberia ambaye siku zote hupenda kutania timu katika ligi zote anazochambua anasema kwamba “ubingwa wa Arsenal unatarajia mkosi wa Man City lakini kujipa afueni ya kumaliza kwa uhakika katika nafasi ya pili kunahitaji angalau pointi mbili kati ya zote sita itakuwa ikiwania katika mechi hizo mbili iliyo nazo”.

Liverpool inangojea kumaliza udhia na Tottenham Hotspur kuanzia saa kumi na mbili jioni, Aston Villa mnamo Mei 13 na kisha Wolves mnamo Mei 19.

Kwa upande mwingine, Man City inatazamia kuwinda ubingwa kupitia vipute dhidi ya Fulham mnamo Mei 11, Tottenham mnamo Mei 14 na hatimaye West Ham United mnamo Mei 19, 2024.

  • Tags

You can share this post!

Kocha Jurgen Klopp kagombana na hawa wachezaji sita

Natafuta mwanamke mwaminifu nimuoe, je, nitampata?

T L