• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Presha kwa KCB inapotafuta umalkia wa voliboli

Presha kwa KCB inapotafuta umalkia wa voliboli

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya kutumia fedha nyingi kuimarisha kikosi chake mwezi Desemba mwaka 2018, klabu ya KCB ina presha inapofukuzia taji lake la kwanza kabisa la Ligi Kuu ya Voliboli ya kinadada itakayoingia mkondo wa lala-salama katika ukumbi wa kimataifa wa Kasarani mnamo Novemba 22-24, 2019.

Wanabenki hao, ambao watalimana na timu ya DCI katika mechi ya kwanza Ijumaa, ilinyakua kocha wa timu ya taifa Japheth Munala pamoja na wachezaji nyota Leonida Kasaya, Noel Murambi na Violet Makuto, na Christine Njambi, Veronica Kilabat, Jemima Siangu na Truphosa Chepkemei. Pia, ilitafuta huduma za mshambuliaji matata wa Rwanda Ernestine Akimanizanye.

Vipusa wa Munala wataingia awamu hii inayohusisha timu zilizokamilisha msimu wa kawaida katika nafasi nne za kwanza, na presha kali ya kuonyesha kuwa iliwekeza vyema.

Timu ya KCB ilizamia maandalizi makali ya wiki moja katika ukumbi wa Nyayo pamoja na uwanja wao wa KCB mtaani Ruaraka.

Munala pia amepigwa jeki na chipukizi matata Belinda Barasa kutoka akademia ya KCB.

Baada ya kibarua cha DCI, timu ya KCB itavaana na mabingwa watetezi Kenya Prisons hapo Jumamosi na kukamilisha kampeni Jumapili dhidi ya mabingwa wa zamani Kenya Pipeline.

KCB na Pipeline sasa ni mahasimu wakuu. Hii ni baada ya Pipeline kupokonywa wachezaji saba pamoja na Munala mwezi Desemba mwaka 2018.

Mechi kati ya KCB na DCI itataunguliwa na ile inayokutanisha Prisons na Pipeline hapo saa nne asubuhi leo.

Klabu ya jeshi la polisi (GSU), Ulinzi (KDF), Halmashauri ya Bandari za Kenya (KPA) na Kenya Prisons pia zitawania taji la wanaume kuanzia leo hadi Jumapili.

Washindi na nambari mbili kutoka vitengo hivyo viwili watafuzu kuwakilisha Kenya katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2019 nchini Misri.

Mbali na kuwa benki ya KCB ina timu ya wanawake, pia ndio mdhamini mkuu wa mashindano haya ya timu nne-bora.

  • Tags

You can share this post!

Vijana wahimizwa kukuza talanta zao

KIKOLEZO: Walichepuka ila haikuwa ishu!

adminleo