Michezo

Presha kwa Oktay mashabiki wa Gor wakitaka atimuliwe

January 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa Gor Mahia wanamlia Kocha Mkuu Hassan Oktay wakitaka afurushwe kabla ya chombo cha mabingwa hawa mara 17 wa Kenya kuzama.

Mturuki huyu, ambaye aliajiriwa na Gor mnamo Desemba 10 mwaka 2018 baada ya Muingereza Dylan Kerr kuondoka, amejipata pabaya kufuatia klabu yake kutoka sare ya 1-1 dhidi ya mabingwa wa mwaka 2008 Mathare United uwanjani Kasarani mnamo Januari 6, 2019.

Hii ilikuwa mechi yake ya tano kwenye Ligi Kuu. Katika matokeo ya kwanza ligini, Gor ilishinda Zoo Kericho (4-0) na Chemelil Sugar (2-0), ikapoteza dhidi ya Kariobangi Sharks (1-0) na kukabwa na Mathare 1-1 tangu awasili. Alishikilia usukani Gor ikibanduliwa nje ya Klabu Bingwa Afrika kwa bao la ugenini baada ya kupigwa 2-0 na Lobi Stars nchini Nigeria katika mechi ya marudiano mnamo Desemba 22. Gor ilikuwa imelima Lobi 3-1 jijini Nairobi hapo Desemba 16.

Baada ya kutoka 1-1 dhidi ya Mathare, mashabiki hawakuwa na maneno mazuri kwa Oktay. Shabiki Kenyanitoe Martinez alisema, “Gor inafaa kutafuta kocha mpya. Kocha huyu aliletwa kutoka klabu aliyohudumu kama naibu wa kocha na timu hiyo ilimaliza ligi katika nafasi ya pili kutoka mkiani kwa hivyo hawezi kuleta ufanisi. Itakuwa afueni akifukuzwa mapema.”

Mwangi Julius Mburu anaomba Kerr arejee K’Ogalo. “Dylan Kerr rudi uokoe Gor Mahia. Hassan Oktay anachemsha. Tunakuomba urejee kwa sababu mambo yanavyoonekana tutashushwa ngazi. Oktay aende ama tuendelee kulia. Hawezi kutupeleka popote. Tunavyoendelea kumpa muda ndivyo tutaumia.”

Naye Steven George anasema, “Tafadhali fukuzeni huyu kocha na mlete kocha anayechukulia kazi kwa uzito.” Maoni kama haya yalitolewa na mashabiki wengi kwenye mitandao ya kijamii wakiwemo Mak Okwirry Owuor, Brio Afric Lethal na Tarzan Johnso.

Baada ya sare hii, Gor inashikilia nafasi ya nane kwa alama saba kutokana na mechi tano nayo Mathare inaongoza ligi hii ya klabu 18 kwa alama 14 baada ya kusakata mechi sita. Mechi ijayo ya Gor ni dhidi ya Posta Rangers mnamo Januari 9 nayo Mathare italimana na Tusker hapo Januari 12.