• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Presha Tottenham Hotspur na Arsenal zikionana

Presha Tottenham Hotspur na Arsenal zikionana

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

MAJIRANI Tottenham Hotspur na Arsenal watafufua uhasama wao leo Jumamosi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, huku kila mmoja wao akikabiliwa na presha.

Spurs, ambayo inashikilia nafasi ya tatu, itakuwa mwenyeji wa nambari nne Arsenal uwanjani Wembley zikipigania tiketi ya kuingia Klabu Bingwa Ulaya kwa kumaliza ligi katika mduara wa nne-bora dhidi ya nambari tano Manchester United na nambari sita Chelsea.

Wiki moja iliyopita, ndoto ya Tottenham kuwania taji ilikuwa hai, lakini vichapo dhidi ya Burnley na Chelsea sasa vimehatarisha nafasi yao katika mduara wa klabu nne-bora wanapojiandaa kualika Arsenal.

Pengo kati ya Spurs na Arsenal lilipungua hadi alama nne baada ya vijana wa Mauricio Pochettino kulemewa na Chelsea nayo Arsenal ya Unai Emery ikapepeta Bournemouth 5-1. United na Chelsea pia haziko mbali katika maeneo ya kufuzu kushiriki Klabu Bingwa msimu ujao.

Kuharibu mambo hata zaidi ni kwamba Spurs haijarudiana na viongozi Liverpool na nambari mbili Manchester City katika orodha ya mechi zao 10 zilizosalia.

Pochettino hajachoka kusifu vijana wake kwa juhudi za kusalia katika mbio hizi kwa muda mrefu hasa baada ya kuandikisha ushindi katika dakika za lala-salama dhidi ya Fulham, Watford na Newcastle bila kuwa na mvamizi matata Harry Kane aliyekuwa mkekani.

Nahodha huyu wa Uingereza amerejea kikosini, lakini licha ya kukabiliana na uchovu kutokana na Kombe la Dunia na kuandamwa na orodha ndefu ya majeraha, Spurs haikununua mchezaji na imelazimika kuishi Wembley, makao ambayo si yake, uwanja wake wa White Hart Lane ukipanuliwa. Huenda Spurs inaishiwa pumzi wakati mbaya.

Pochettino anaamini Arsenal pia inakabiliwa na presha, hasa ya kutafuta kuepuka msimu wa tatu mfululizo bila kuwa katika Klabu Bingwa Ulaya.

Mojawapo ya matokeo mazuri kabisa Unai Emery ameandikisha katika mwaka huu wake wa kwanza Arsenal ni kupiga Tottenham 4-2 mapema Desemba mwaka jana.

Hata hivyo, licha ya ushindi huo uwanjani Emirates na zingine uwanjani humu, Mhispania huyu hajavumbua mbinu ya kushinda ugenini. Arsenal imeshinda ugenini mara moja pekee ligini katika mechi saba zilizopita na ushindi huo ulipatikana dhidi ya wavuta-mkia Huddersfield.

Mesut Ozil na Henrikh Mkhitaryan waling’aa walipoanza mechi ya ligi pamoja kwa mara ya kwanza Jumatano tangu Novemba 2018, huku nguvu-mpya Alexandre Lacazette akihitimisha kuchana nyavu baada ya Pierre-Emerick Aubameyang anayeongoza kuifungia mabao kupachika bao lake la 19 msimu huu.

Naye Pep Guardiola amemtaka Riyad Mahrez kujitokeza kwa nguvu kusaidia kampeni ya Manchester City inayolenga mataji manne. Mahrez ni mchezaji ghali wa City. Alinunuliwa kwa Sh7.9 bilioni. City itapata fursa nzuri ya kuchukua usukani kutoka kwa Liverpool itakapomenyana na Bournemouth leo. Liverpool italimana na Everton hapo kesho.

Naye Ole Gunnar Solskjaer anatumai mshambuliaji Romelu Lukaku yuko tayari kuchukua nafasi ya kutegemewa kwa mikono miwili. Mbelgiji huyu alianza kuonyesha ukatili uliokuwa umepiga chenga alipopachika mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Crystal Palace.

  • Tags

You can share this post!

Rashid Echesa: Waziri aliyetemwa nje

USHAIRI WENU: Kazi nitazochapa

adminleo