PSG bila nyota wake wakuu yalipiza kisasi dhidi ya Real Madrid
PARIS, Ufaransa
ANGEL Di Maria alimiminiwa sifa tele baada ya kufuma wavuni mabao mawili, huku Paris Saint-Germain ikilipiza kisasi dhidi ya waajiri wake wa zamani Real Madrid 3-0 bila huduma za Neymar na Kylian Mbappe katika ngarambe ya Klabu Bingwa Ulaya, Jumatano.
Di Maria alimwaga kipa Thibaut Courtois karibu na mlingoti na kuweka PSG bao 1-0 juu dakika ya 14 uwanjani Parc des Princes, lakini bao lake la pili baada ya nusu saa ndilo lilileta msisimko kwenye mechi hii.
Raia huyo wa Argentia, ambaye aling’ara akichezea Real kwa miaka minne na kushinda Kombe la Klabu Bingwa nayo mwaka 2014 kabla ya kuhamia Manchester United, aliacha Courtois hoi na shuti kali kupitia mguu wake wa kushoto kutoka nje ya kisanduku.
Thomas Meunier alipachika bao la dakika ya mwisho, lakini ni Di Maria, ambaye alikuwa ameongoza maangamizi hayo, akajaza mapengo yaliyoachwa baada ya Mbappe na Edinson Cavani kujeruhiwa pamoja na Neymar kutumikia marufuku ya mechi mbili aliyopokea alipotusi maafisa wa mechi wakati PSG ilichapwa na Manchester United 3-1 katika mechi ya raundi ya 16-bora.
“Hatushangazwi sana kwa sababu amekuwa akionyesha ukatili langoni kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa,” alisema kocha wa PSG, Thomas Tuchel. “Alikuwa shujaa leo usiku. Yeye huwa hatari.”
Baada ya likizo kutawaliwa na tetesi za iwapo Neymar ataondoka uwanjani Parc des Princes, mchezo wa Di Maria ulikuwa wa kuwakumbusha wapinzani kuwa mabingwa hao wa Ufaransa wana wachezaji wengine walio na uwezo wa kushinda mechi kubwa kama hizo.
Klabu hizi mbili zinajaribu kurejesha sifa baada ya kuwa na kampeni za kusikitisha barani Ulaya msimu uliopita. Hata hivyo, matokeo haya pia ni kisasi kitamu dhidi ya Real, ambayo PSG 3-1 jijini Madrid na kuilemea 2-1 jijini Paris katika mechi za raundi ya 16-bora mapema mwaka jana.
Vijana wa Tuchel wanasalia na rekodi ya kutoshindwa katika mechi za makundi za Klabu Bingwa tangu mwaka 2004 na tayari wamedhibiti Kundi A kabla ya kukutana na Galatasaray na Club Brugge, ambao walikabana 0-0 Jumatano.
“Kila mtu alikuwa akisema tutawezaje kushinda bila wachezaji hawa wote, lakini inaonyesha hatukutarajiwa kushinda na inaweza kukusaidia unapokuwa bila shinikizo,” aliongeza Tuchel.
Real bado haijaridhisha tangu Zinedine Zidane arejee kuiongoza kwa mara ya pili. Bado kuna kazi kubwa ya kufanywa na mabingwa hawa mara 13 kuenda mbali katika mashindano haya baada ya kubanduliwa nje na Ajax katika raundi ya 16-bora msimu uliopita.
Bao la Gareth Bale lilikataliwa kwa kunawa mpira baada ya teknolojia ya VAR kutumiwa kutoa uamuzi Real ilipojipata mabao 2-0 chini. Sajili mpya Eden Hazard pia hakutoa mchango katika mechi aliyoanza tangu atue uwanjani Santiago Bernabeu kutoka Chelsea katika kipindi kirefu cha uhamisho.
Madrid pia ilikosa huduma za Sergio Ramos, Nacho na Marcelo katika safu ya ulinzi na mwanasoka bora duniani Luka Modric katika safu ya kati.