Michezo

PSG kumsajili Dele Alli baada ya kubanduka Spurs mnamo Januari 2021

December 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) watajaribu tena kumsajili kiungo mvamizi wa Tottenham Hotspur, Dele Alli mnamo Januari 2020.

Miamba hao wa Ufaransa walijaribu kujinasia huduma za nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 mwishoni mwa msimu wa 2019-20 ila mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy, akazuia uhamisho huo.

Mustakabli wa Alli kambini mwa Spurs umezidi kuzingirwa na wingu jeusi huku akichezeshwa na kocha Jose Mourinho katika kikosi cha kwanza mara moja pekee katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2020-21. Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza muhula huu ambapo Spurs walipigwa 1-0 na Everton waliokuwa ugenini.

Tangu Oktoba 4, 2020 alipowajibishwa dhidi ya Manchester United katika ushindi wa 6-1 uliosajiliwa na Spurs, Alli hajawahi kuvalia tena jezi za waajiri wake katika mchuano wowote.

Licha ya kupangwa katika kikosi cha wanasoka wa akiba dhidi ya Royal Antwerp ya Ubelgiji katika Europa League mnamo Disemba 10, 2020, Alli hakuchezeshwa katika gozi hilo lililoshuhudia Spurs wakishinda 2-0 ugenini.

Katika jumla ya mechi 230 ambazo Alli amechezea Spurs hadi kufikia sasa, nyota huyo amefunga mabao 64 na kuchangia mengine 56.

Ingawa wingi wa visa vya majeraha kambini mwa Spurs huenda ukamshuhudia akirejea katika kikosi cha kwanza, wakala wa sogora huyo ameshikilia kwamba Alli ataagana na waajiri wake wa sasa mnamo Januari 2021.