PSG wabanwa na Bordeaux ligini kabla ya kurudiana na Manchester United kwenye UEFA
Na MASHIRIKA
VIONGOZI wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), PSG, walilazimishiwa sare ya 2-2 na Bordeaux mnamo Novemba 28, 2020 siku tatu kabla ya kufunga safari ya Uingereza kwa minajili ya kurudiana na Manchester United kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ugani Old Trafford.
Neymar Jr alisawazishia PSG kupitia penalti alipofunga bao lake la 50 katika soka ya Ligue 1 kunako dakika ya 27. Hii ilikuwa baada ya Timothee Pembele kujifunga na kuwapa Bordeaux waliokuwa wakicheza ugenini uongozi wa 1-0 katika dakika ya 10.
Moise Kean alifunga bao la pili la PSG katika dakika ya 28 kabla ya Yacine Adli kusawazisha katika dakika ya 60. Bao la Kean lilikuwa lake la sita tangu aingie katika sajili rasmi ya Everton baada ya kuagana na Everton ya Uingereza kwa mkopo.
PSG kwa sasa wamepoteza alama tano muhimu kwenye michuano miwili iliyopita ligini. Ingawa hivyo, kikosi hicho cha kocha Thomas Tuchel bado kinaselelea kileleni mwa jedwali la Ligue 1 kwa alama 25, tatu zaidi kuliko nambari Lille ambao watakuwa wageni wa Saint-Etienne usiku wa Novemba 29, 2020.
Bordeaux walisalia katika nafasi ya 11 kwa alama 16 sawa na Metz na Angers.
PSG watakuwa wageni wa Man-United kwenye gozi la UEFA mnamo Disemba 2, 2020 huku pengo la alama tatu likitamalaki kati yao na masogora hao wa kocha Ole Gunnar Solskjaer ambao wanaongoza msimamo wa Kundi H zikisalia mechi mbili zaidi za hatua ya makundi.
PSG ambao walikuwa wanafainali wa UEFA mnamo 2019-20 sasa wanajivunia alama sawa na nambari tatu Leipzig kwenye Kundi H. Leipzig ya Ujerumani watakuwa wageni wa Istanbul Basaksehir ya Uturuki kwenye mchuano mwingine wa Kundi H mnamo Disemba 2, 2020.