PSG yazima ndoto ya Atalanta ya Italia
Na CHRIS ADUNGO
PARIS Saint-Germain (PSG) walifunga mabao mawili ya dakika za mwisho na kuiondoa Atalanta ya Italia kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti 12, 2020.
Ufanisi huo wa PSG katika mechi hiyo iliyochezewa jijini Lisbon, Ureno uliwakatia tiketi ya nusu-fainali za UEFA kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25.
Miamba hao wa soka ya Ufaransa watakutana sasa na mshindi wa robo-fainali nyingine kati ya RB Leipzig ya Ujerumani na Atletico Madrid kutoka Uhispania. Gozi hilo la hatua ya nne-bora litatandaziwa jijini Lisbon mnamo Agosti 18, 2020.
Atalanta waliowekwa kifua mbele na fowadi Mario Pasalic katika dakika ya 26, walishikilia uongozi wao wa bao hadi dakika ya 90 ambapo Neymar Jr alishirikiana vilivyo na Marquinhos aliyewarejesha PSG mchezoni.
Mvamizi chipukizi Kylian Mbappe aliyetokea benchi katika kipindi cha pili, alichangia bao la pili la PSG ambalo lilijazwa kimiani na mshambuliaji wa zamani wa Stoke City, Eric Maxim Choupo-Moting sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.
PSG waliokuwa wakiadhimisha miaka 50 ya kuasisiwa kwao, walianza mchuano kwa matao ya chini huku Neymar pekee akiwa mchezaji aliyeonakana kutawaliwa na kiu ya kufungia bao kikosi hicho cha mkufunzi Thomas Tuchel.
Ilikuwa hadi dakika ya 66 ambapo kasi ya mechi ilibadilika baada ya ujio wa Mbappe aliyeshirikiana vilivyo na Neymar.
Utepetevu wa PSG katika mechi za UEFA umekuwa ukidhihirika katika misimu ya hivi karibuni, tukio linalosalia kudhihirisha hilo ni lile lililoshuhudia Barcelona wakitoka chini kwa mabao 4-0 katika hatua ya 16-bora na hatimaye kuwabandua mnamo 2017.
Ulegevu huo wa PSG hasa katika hatua muhimu za kivumbi hicho umechangia kufutwa kazi kwa wakufunzi Unai Emery, Carlo Ancelotti na Laurent Blanc kambini mwa wafalme hao wa soka ya Ufaransa.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Atalanta kunogesha kipute cha UEFA msimu huu na mafanikio hayo ya kutinga robo-fainali inatazamiwa kuwaaminisha hata zaidi katika kampeni za msimu ujao wa 2020-21. Atalanta waliambulia nafasi ya tatu kwenye ni kampeni za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu huu kwa alama 78 sawa na Lazio.