Michezo

Pufya: Kando na Pogba, wafahamu wanasoka waliowahi kufungiwa nje

March 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

KUPIGWA marufuku kwa mwanasoka Paul Pogba wa klabu ya Juventus inayoshiriki Ligi Kuu ya Serie A nchini Italia, kumeibua kumbukumbu kuhusu wanasoka wengine ambao wameshawahi kupigwa marufuku kwa kupatikana na kosa la kutumia dawa za kuongeza nguvu miili na misuli yao.

Pogba alipigwa marufuku kucheza soka kwa muda wa miaka minne na Jopo la Kuchunguza Utumiaji Dawa za Kuipa Nguvu Miili (NADO) la Italia, baada ya kupatikana na kosa la kutumia dawa hizo.

Kutokana na marufuku hiyo, hilo linamaanisha kuwa mwanasoka huyo, 30, atarejelea uchezaji soka 2027 akiwa na umri wa miaka 30.

Licha ya marufuku hiyo kuzua gumzo katika ulimwengu wa soka, mwanakandanda huyo si wa kwanza kuwahi kupigwa marufuku kwa kosa kama hilo.

Darubini ya Taifa Spoti imerejesha jicho lake nyuma na kuwaangazia wanasoka wengine ambao washawahi kupigwa marufuku au kusimamishwa kwa muda kucheza soka, baada ya kupatikana na kosa kama hilo.

Baadhi ya wanasoka hao ni Deco, Samir Nasri, Kolo Toure, Edgar Davids, Adrian Mutu, Pep Guardiola kati ya wengine wengi.

Mnamo 2011, Kolo Toure alisimamishwa kucheza kandanda kwa muda wa miezi sita, baada ya kupatikana na kosa la kutumia dawa za kuipa nguvu misuli yake.

Kolo ni kakake kiungo wa kati wa zamani wa timu ya Manchester City, Yaya Toure. Kutokana na hilo, klabu hiyo ililazimika kujaza nafasi yake na mwanasoka Joleon Lescott. Hata hivyo, katika kujitetea kwake, alisema kuwa alimeza tembe za mkewe bila kujua.

Mwanasoka Edgar Davids anakumbukwa kwa nywele zake aina ya ‘dreadlocks’. Mnamo 1998, alitoka klabu ya AC Milan na kujiunga na Juventus. Hata hivyo, alipatikana kutumia dawa za kumwongeza mwilini mnamo 2001. Alipatikana akitumia dawa aina ya Nandrolene.

Mwanasoka Adrian Mutu alipatikana akitumia dawa hizo mnamo 2004 alipokuwa katika klabu ya Chelsea. Mwanasoka huyo alipatikana tena akitumia dawa hizo alipokuwa katika klabu ya Fiorentina, Italia. Katika tukio la Chelsea, alipigwa marufuku kwa muda wa miezi sita baada ya kupatikana akitumia dawa aina ya Cocaine. Mnamo 2010 katika klabu ya Fiorentina, alipatikana akitumia dawa aina ya Sibutramine.

Licha ya kuiwezesha klabu ya Manchester City kupata ushindi mkubwa msimu uliopita, kocha Pep Guardiola pia ashawahi kusimamishwa kucheza soka baada ya kupatikana akitumia dawa za kujitutumua.

Guardiola alipatikana akitumia dawa hizo mnamo 2001, alipojiunga na klabu ya Brescia nchini Italia. Hii ni baada ya kandarasi yake katika klabu ya Barcelona kukamilika. Baada ya sampuli za damu yake kuchunguzwa, alipatikana akitumia dawa aina ya Nandrolone. Hata hivyo, aliondolewa madai hayo yote baada ya kuwasilisha rufaa mwaka 2009.