Michezo

Punguza mshahara uhamie Uhispania, Kepa aambiwa

July 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KIPA mzawa wa Uhispania, Kepa Arrizabalaga yuko radhi kupungiziwa mshahara kwa hadi asilimia 30 ili kufanikisha uhamisho wake hadi Sevilla au Atletico Madrid ilmuradi tu aepukane na dhihaka za mashabiki wa Chelsea.

Mlinda-lango huyo alielekezewa zigo la lawama mnamo Julai 22, 2020 baada ya utepetevu wake kuwaruhusu mabingwa Liverpool kuwafunga jumla ya mabao matano katika ushindi wa 5-3 ugani Anfield.

Kushambuliwa kwa Kepa ambaye aliandikiwa jumbe nyingi za matusi mitandaoni, kunajiri majuma machache tu baada ya kocha Frank Lampard kumrejesha katika kikosi cha kwanza.

Kepa, 25, aliwahi kutemwa kabisa na Lampard katika kikosi cha kwanza cha Chelsea mwanzoni mwa msimu huu baada ya kisu cha makali yake kusenea.

Hatua hiyo ilizua tetesi kuhusu uwezekano wa Chelsea kutafuta mrithi wa Kepa katika soko la uhamisho ambalo linafunguliwa rasmi Julai 27 hadi Oktoba 5, 2020.

Kepa, ambaye kwa sasa hupokea mshahara wa Sh21 milioni kwa wiki ndiye kipa ghali zaidi duniani kwa sasa. Kipa huyo yuko katika mwaka wa pili pekee katika mkataba wake na Chelsea, na hilo ni jambo linalofanya vikosi vingi kushindwa kumudu bei yake iwapo Lampard atapania kabisa kumtema ugani Stamford Bridge.

Mnamo Januari 2020, Kepa alihusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua Atletico katika mpango ambao ungemshuhudia kipa Jan Oblak akiagana na kocha Diego Simeone na kuchukua nafasi ya Kepa ugani Stamford Bridge.

Chelsea waliweka mezani kima cha Sh10 bilioni mnamo 2018 kwa minajili ya huduma za Kepa aliyeagana rasmi na kikosi cha Athletic Bilbao nchini Uhispania.

Idadi kubwa ya mabao ambao Chelsea wamefunga msimu huu, yakiwemo matano kutoka kwa Liverpool, ni jambo ambalo linatarajiwa kumchochea Lampard kutafuta kipa mpya atakayemtegemea katika kampeni za msimu ujao.

Mbali na kumvizia Oblak, Chelsea wanahemea pia maarifa ya kipa Nick Pope wa Burnley na Den Henderson ambaye kwa sasa anawadakia Sheffield United kwa mkopo kutoka Manchester United.

Chelsea waliwahi pia kuwatuma maskauti wao kumtazama uwanjani kipa wa Borussia Dortmund, Roman Burki kabla ya mlinda-lango huyo mzawa wa Uswisi kutia saini mkataba mpya wa miaka mitatu mnamo Juni 19, 2020.