Michezo

PWANI: Uwanja wa Tononoka kukarabatiwa uwafae wanasoka

June 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MARA baada ya wauzaji bidhaa kuondoka uwanja wa Tononoka na kurudi Kongowea, Serikali ya Kaunti ya Mombasa imewatuliza nyoyo mashabiki wa soka wa Pwani kwa ahadi ya kuukarabati uwanja huo urudi kutumika kwa mechi za mchezo huo wa mpira wa miguu.

Afisa Mkuu wa Michezo wa Kaunti ya Mombasa, Innocent Mugabe alipozuru sehemu hiyo alithibitisha kuwa uwanja wa Tononoka utabakia kutumika kwa mchezo wa soka na kwamba serikali itaukarabati uwe mzuri kuliko ulivyokuwa hapo awali.

Mugabe aliwahakikishia mashabiki wa kandanda kuwa uwanja wa Tononoka utabakia kutumiwa kwa mchezo wa mpira wa miguu baada ya kutumika kama soko kwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja unusu.

“Tuliutumia uwanja huo kwa sababu ya kuondoa msongamano katika soko la Kongowea lakini hivi sasa tumewaambia wauzaji warudi huko na tunaanza kazi ya kuurekebisha uwanja huu ili urudi kutumika kwa mazoezi na mechi,” akasema Mugabe.

Akiwa uwanjani hapo pamoja na Afisa wa Uwanja wa Kaunti ya Mombasa, Abdulhalim Abdulrahman Kiduwazi, Mugabe alisema watazungusha seng’enge katika uwanja huo na kuutengeneza kwa kupanda nyasi kabla ya kutumika kwa mazoezi na mechi.

“Tutaondoa saruji uwanjani na kuujenga upya kwa kupanda nyasi. Ninawahakikishia utakuwa mzuri kuliko ulivyokuwa kabla ya wauzaji bidhaa kuwa hapo,” akasema afisa huyo wa michezo aliyekuwa uwanjani kuhakikisha taka zote zilizobakia zimezolewa.

Hali mbovu ya uwanja wa Tononoka ilileta malalamiko mengi na hasa kutoka kwa mwanasiasa Ali Mwatsahu ambaye aliitaka serikali ya kaunti hiyo pamoja na serikali kuu waununue uwanja huo kama unamilikiwa na watu binafsi.

Mwanasiasa Ali Mwatsahu akilalamika na kuonyesha saruji iliyokuwa akiwekwa uwanja wa Tononoka. Picha/Abdulrahman Sheriff

Mugabe alisema watafanya bidii kwa kipindi kifupi kuona uwanja huo umerudi kutumiwa kwa mechi za kandanda kama kawaida yake.

“Tunaondoa uchafu wote pamoja na kuondoa saruji iliyowekwa na tuanze kupanda manyasi uwanjani,” akasema.

Mwanasiasa Ali Mwatsahu alisema amefurahikia kuona wachuuzi wameondoka uwanjani hapo lakini angali ana wasiwasi kama kuondoka kwao kutaifanya serikali ya Kaunti ya Mombasa iurudishe uwanja huo kutumika kwa mazoezi na mechi za ligi mbalimbali.

“Nimefurahia hili lakini muhimu zaidi ni pale nitashuhudia uwanja huu ukirekebishwe urudi hali ya kuweza kutumika kwa mechi kuchezwa,” akasema Mwatsahu.

Alisema alishangaa kuona uwanja huo ukitiwa saruji wakati wahusika wa kufanya kitendo hicho wanafahamu vizuri kuwa uwanja huo unawafaa maelfu ya wachezaji na hasa vijana katika kuinua vipaji vya uchezaji wao.

Mwatsahu alirudia ombi lake la kutaka uwanja huo ubakie kutumika kwa mpira wa miguu kwani kutumika kwa mambo mengine yoyote, kutawanyima vijana fursa ya kufanikiwa kwa malengo yao ya kuinua vipaji vyao ili wafanikiwe kucheza soka la kulipwa.

“Sharti ieleweke kuwa uwanja huu wa Tononoka umewahi kutoa wanasoka wengi waliokuwa na majina makubwa miaka mingi iliyopita na hadi sasa baadhi ya wale wanaochezea timu kubwa hapa nchini, wamepitia kucheza katika uwanja huu,” akasema.

Mwatsahu alisema kama uwanja huo ni wa mtu binafsi, serikali ya kaunti ama serikali kuu iununuwe ili ubakie kuwa mikononi mwa wananchi na vijana zaidi wapate kuinua vipaji vya uchezaji wao.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Cosmos FC, Aref Baghazally amepongeza uamuzi wa kuwaondoa wachuuzi na kutaka ahadi hiyo ya kuujenga upya uwanja huo wa Tononoka itimizwe ili mechi za ligi za msimu ujao zipate kuchezwa uwanjani humo.

“Ahadi ya Mugabe kuwa watapanda nyasi katika uwanja huo ni ya kupongezwa. Tunaamini jambo hilo litatimizwa kwa sababu litawafaa vijana wetu kuendeleza vipaji vya uchezaji wao,” akasema Baghazally.