Raha Kenya Police ikihitaji ushindi moja tu kutwaa KPL
KENYA Police Jumapili walikaribia kuandika historia ya kushinda taji la Ligi Kuu (KPL) baada ya kuwahi ushindi wa 1-0 dhidi ya FC Talanta kwenye uga wa Kenyatta, Kaunti ya Machakos.
Nafasi ya Kenya Police kutwaa ubingwa iliimarishwa na hali kwamba wapinzani wao wa karibu Tusker na Gor wote walidondosha alama.
Tusker walipigwa 7-1 na Sofapaka katika uga wa Dandora, Nairobi huku mabingwa watetezi Gor Mahia wakikabwa sare tasa na Murangá Seal wanaopambana kusalia KPL. Mechi kati ya Gor na Murangá Seal ilichezwa uwanja wa SportPesa Arena Murangá.
Baada ya raundi 32 ya mechi za KPL, Kenya Police wanaongoza kwa alama 61, alama sita mbele ya Tusker huku Gor ikiwa nambari tatu kwa alama 54. Gor bado imesalia na mechi moja ya akiba.
Kushinda taji lao la kwanza la KPL, Kenya Police wanahitaji tu kushinda mechi moja ambayo itakuwa dhidi ya Shabana na Gor.
Ushindi dhidi Shabana au Gor utahakikisha kuwa wanafikisha alama 64 ambapo hawawezi kufikiwa hata K’Ogalo au Tusker zikishinda mechi zao zote.
Tusker imesalia na mechi dhidi ya Kariobangi Sharks na Kakamega Homeboyz mtawalia. Gor imebaki na Debi ya Mashemeji dhidi ya AFC Leopard kisha Ulinzi Stars kabla ya kumaliza msimu na Kenya Police.
Kwenye mechi nyingine ya KPL, Kakamega Homeboyz ilipiga Sharks 2-1 uga wa Dandora nao Mara Sugar ikashangaza Shabana 1-0 ugani Gusii.
Nairobi City Stars iliagana sare ya 1-1 na Posta Rangers ugani Kenyatta kisha Bandari ikaagana sare tasa na AFC Leopards ugani Mbaraki Kaunti ya Mombasa.
Kwenye mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu, mvamizi wa Kakamega Homeboyz Moses Shumah aliongeza idadi ya mabao yake hadi 17 baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Sharks.
Kuelekea mechi za Jumapili, Shumah na mvamizi wa FC Talanta Emmanuel Osoro walikuwa wamefunga mabao 16. Hata hivyo, Osoro hakufunga jana dhidi ya Kenya Police.
Goli la dakika ya 15 kutoka kwa David Simuyu lilitosha kuwapa Kenya Police ushindi dhidi ya FC Talanta na kuimarisha nafasi yao ya kutwaa taji la FKF-PL msimu huu.